Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kinakamilisha mfumo wa dirisha la pamoja la kuhudumia wawekezaji la kielektroniki Tanzania (TeIW) ili kumwezesha mwekezaji kujisajili popote duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Bw. Gilead Teri alisema Jijini Dar es Salaam hivi karibu kuwa mfumo huo ambao upo kwenye hatua za mwisho kukamilika utamuondolea mwekezaji usumbufu kwani ataweza kupata huduma zote zinazotolewa na taasisi saba.
“Mfumo huu utaokoa muda kwa mwekekezaji kuja moja kwa moja TIC kwani popote alipo anaweza kujisajili na kutuma maombi ya vibali, leseni na kupata cheti kwa haraka endapo akidhi vigezo vinavyohitajika kwa njia ya kielektroniki,” alisema Bw. Teri pembezoni mwa Kikao maalumu cha Kamati Tendaji ya Baraza la Biashara la Taifa.
Bw. Teri alizitaja taasisi hizo ambazo zipo kwenye mfumo kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), BRELA, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Ardhi na TIC yenyewe.
“Mfumo huu ni hazina ya taarifa zote muhimu kwa ajili ya uwekezaji kwa wadau wote wanaohitajika kuwekeza hapa nchini.Maboresho haya yote juhudi ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekusudia kuifungua nchi,” alisema Bw. Teri.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa TIC, kupitia mfumo huo mwekezaji hatalazimika kufika kwenye ofisi za taasisi hizo saba kwani kila kitu atakuwa amekalimisha kwenye mfumo.
“Uwepo wa mfumo huu ni mkombozi kwa wawekezaji wa ndani na wale wawekezaji wa kutoka kwani utamrahisishia mwekezaji kusajili uwekezaji wake kwenye kituo,” alisema Bw. Teri na kuongeza kuwa kituo kimejipanga kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kujenga uchumi imara.
Alisema mfumo unaotumika sasa ni ule ambao mwekezaji anaweza kuja ofisini akaleta maombi na yakafanyiwa kazi na zile taasisi saba kwani mfumo wa electronic upo katika hatua za mwisho za matengenezo.
“Kwa sasa tupo kwenye hatua ya majaribio baada ya mwezi huu (Mei) mfumo huu utakuwa tayari kwa matumizi.Nawaomba watanzania kutembelea tovuti ya TIC ambayo ni www.tic.go.tz,” alisema Bw. Teri.
Miaka miwili chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassani, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo mazingira mazuri ya kufanya biashara sambamba na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Serikali ya awamu sita imeazimia kuijenga sekta binafsi imara ambayo itatoa mchango stahiki katika uchumi wa taifa ikiwemo kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali sambamba na kuinua maisha ya watanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...