Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Watumishi
wote wa Mhimili huo kwa utekelezaji thabiti wa Mpango Mkakati na
Programu za Maboresho zinazolenga kuboresha huduma za utoaji haki
nchini.
Mhe.
Prof. Juma ameyasema hayo mapema leo tarehe 18 Mei, 2023 wakati
akifungua Kikao cha siku mbili cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama
ya Tanzania kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF jijini
Dodoma.
“Kabla
sijafungua kikao hiki muhimu, nitakosa fadhila na uungwana kama
nitashindwa kuchukua nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi kwa ufanisi
ambao umejipambanua katika kufanikisha na kusogeza huduma za utoaji haki
karibu na wananchi,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu amesema ili kuendelea na maboresho ya huduma za Mahakama, Viongozi
hawana budi kutambua nafasi na umuhimu wa Wafanyakazi, kwa
kuwashirikisha kwa namna mbalimbali katika kupanga na kutekeleza kwa
kadri ya uwezo wao.
“Hapa
madhumuni makubwa ni kuleta ufanisi na tija zaidi kazini na pia kuondoa
migongano isiyo ya lazima, kuwashirikisha wafanyakazi ni pamoja na
kuhakikisha kuwa wanaelimishwa mara kwa mara kuhusu masuala yote muhimu
ya Mhimili wa Mahakama yanayojitokeza kila siku,” amesema Mhe. Prof.
Juma.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania amewataka Watumishi hao kusoma
Rasimu ya Taarifa ya REPOA ya Utafiti Kuhusu Kuridhika Kwa Watumiaji wa
Huduma za Mahakama (Court User Satisfaction Survey) 2023.
“Katika
karne hii tuliyo nayo ni muhimu kuwa na desturi ya kujisomea ili
kuendana na mabadiliko ya Teknolojia na vilevile nawaomba hao kuwa na
desturi ya kupenda kujisomea nyaraka mbalimbali zitakazowezesha kujua
zaidi kuhusu maboresho ya kufanya,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.
Jaji
Mkuu amesema, kwa mujibu wa Rasimu ya taarifa hiyo aliyoisoma,
inaonesha kuwa, tathmini ina mwelekeo mzuri ambapo amesema “Kumekuwa na
ongezeko thabiti la kiwango cha kuridhika na wepesi wa kuwasikiliza,
heshima na adabu inayoonyeshwa na wafanyakazi wa mahakama kutoka 2015
hadi 2023.”
Akizungumzia
safari ya maboresho ya Mahakama, Jaji Mkuu amesema TEHAMA imechangia
kwa kiasi kikubwa huku akiendelea kusisitiza kuhusu matumizi ya
Teknolojia kwa vitendo ili kutimiza azma ya kuwa na Mahakama mtandao
(e-Judiciary).
“Ndugu
Wajumbe na wageni waalikwa, naomba nitumie Baraza hili kutambua mchango
mkubwa katika kuleta ufanisi uliotokana na matumizi ya TEHAMA. Nitumie
pia Baraza hili kuendelea kukumbushana kuwa utoaji wa huduma kwa umma
katika Karne ya 21 ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka michache tu
iliyopita,” ameeleza.
Kadhalika,
Jaji Mkuu amesema watumishi wasiridhike na elimu na ujuzi walionao na
badala yake kujiendeleza na kujisomea nje ya taaluma zao ili kuwa na
uwezo wa kufanya kazi nyingi nje ya taaluma iliyowapa ajira
(multi-task).
“Jitihada
binafsi za watumishi ndio zitaiwezesha Mahakama kuhimili pengo kubwa la
idadi ya watumishi. Mahakama inahitaji watumishi 10,351, waliopo ni
6,000, sawa na asilimia 58. Karne ya 21 ni ya ubunifu. Kila mtumishi kwa
nafasi yake, anatakiwa kuwa mbunifu na kuongeza thamani katika kazi
anazofanya,” amesisitiza.
Amesema,
Kikao cha Baraza, ni wakati mzuri wa kubadilishana uzoefu katika
kukabiliana na changamoto, kukumbushana hatua iliyofikiwa tumefika na
kujua wapi panahitaji kujirekebisha pamoja na kuwaelimisha watumishi
kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maslahi na haki zao.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Kikao cha
Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 18 Mei,
2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF jijini Dodoma.
Mtendaji
Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto),
Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) pamoja na
sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania
wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza
hilo, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Picha
za baadhi ya Wajumbe na Wawakilishi wa Wafanyakazi wa Baraza la
Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na
Mwenyekiti wa Baraza hili, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na
meza wakiimba wimbo wa Mshikamano daima wakati wa kikao cha Baraza la
Wafanyakazi kilichoanza leo tarehe 18 Mei, 2023.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama ya Tanzania, Bw. Ezra Kyando akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...