Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo ametembelea Kliniki ya Tiba Saidizi kwa waraibu (Methadone) iliopo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru na kuangalia huduma inayoendelea kutolewa kwenye kliniki hiyo.
Ametembelea Kliniki hiyo leo Juni 27, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuendelea kutoa huduma za tiba kwa Waraibu na kueleza kwamba Maamlaka itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwenye kliniki hiyo
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Mount Meru Dkt. Alex Ernest ameishukuru Mamlaka kwa kuendelea kutoa misaada kwenye kliniki hiyo kuanzia ujenzi wa jengo la kliniki, samani pamoja na vifaa tiba vinavyorahisisha uendeshaji wa huduma hiyo.
Ameongeza kwamba hosptali hiyo imefanikiwa kutenga eneo la mafunzo ya kilimo cha mbogamboga ili kuwasaidia waraibu kupata ujuzi na kutumia kama fursa ya kujipatia kipato.
Awali akisoma risala fupi mbele Kamishna Jenerali , Mkuu wa kitengo cha Methadone Dkt. Salum Said ameeleza Kliniki ya tiba saidizi ya waraibu (Methadone) ni kliniki inayotoa dawa ya Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya kwa Mikoa mitatu.
Ameitaja mikoa hiyo ni Arusha, Kilimanjaro na Manyara na kwa kipindi cha miaka miwili tangu ianzishwe imehudumia waraibu wapatao 616, wanaume wakiwa ni asilimia 82 na wanawake asilimia 18.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...