*Jamii yashauriwa kutumia uwepo wa shamba hilo kujifunza kwa vitendo utunzaji mazingira, ufugaji nyuki

Na Said Mwishehe , Michuzi TV-Geita

IMEELEZWA uwepo wa Shamba la Miti Silayo lililopo wilayani Chato mkoani Geita umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo na mikoa jirani kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali zikiwemo za kujifunza namna bora ya kupanda miti na ufugaji nyuki.

Hayo yameelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kupitia Mhifadhi Patrick Mbungi ambaye pia ni Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu Shamba la Miti Silayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao pamoja na mambo mengine walitaka kufahamu faida za uwepo wa shamba hilo lililozinduliwa rasmi Januari 17,2023.

“Wakati wa uzinduzi wa shamba hili aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Hayati Dk.John Magufuli alibadilisha jina kutoka shamba la miti biharamuro na kuwa Shamba la miti silayo kutokana na utendaji mzuri wa Kamishina wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo,”amesema .

Aidha amesema Shamba la Miti Silayo limeanzishwa kwa malengo ya kukidhi mahitaji ya malighafi kwa wananchi na viwanda lakini kuhakikisha wanaimarisha mazingira na kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yetu .

“Shamba hili limekuwa chanzo kikubwa cha ajira na fursa kwa wananchi wanaopakana na shamba, limekuwa sehemu ya wananchi kujipatia elimu ya namna bora ya utunzaji wa miti, uoteshaji wa miti katika mashamba yao.Katika shamba hili tunajishughulisha hasa na upandaji miti lakini shughuli nyingine ni ufugaji wa nyuki,”amesema Mhifadhi Mbugi.

Amefafanua uwepo wa miti ya Miyombo katika shamba hilo upatikanaji wa nyuki ni mkubwa kwani wanapata chakula cha kutosha ambacho kinasaidia kutengeneza asali ya kutosha inayokidhi mahitaji ya jamii.

“Mbali na kujikita na shughuli za msingi za upandaji miti na ufugaji nyuki tumekuwa tukijihusisha na shughuli za kijamii hasa kusaidia miradi ya maendeleo.Kwa mfano mpaka sasa shamba limesaidia miradi ya ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Nyakayondwa.

“Tumesaidia ujenzi wa ofisi ya walimu katika shule ya sekondari Mikotoni, tumetoa msaada kwa jamii kwa kusaidia ujenzi wa mradi wa maji kwenye Kijiji cha Mtengo na mbali na hapo tumeendelea kutoa elimu ya uteshaji wa miti na namna bora za utunzaji wa mazingira,”amesema Mhifadhi Mbugi.

Ameongeza wamekuwa wakijihusisha moja kwa moja kwenye ugawaji wa miche kwa wananchi ili wajifunze kwa vitendo ni nini maana halisi ya utunzaji mazingira na uhifadhi ya misitu.

Amesisitiza kimsingi uwepo wa Shamba la miti Silayo katika Wilaya ya Chato ni fursa kubwa kwa wananchi kwani shamba hilo limekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira za muda na za mkataba.

Pia amesema kwa utaratibu uliopo huwa wanaruhusu wananchi wanaopakana na shamba kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ambayo wanatarajia kupanda miti kwa namna ya kilimo mseto, hivyo wanapata fursa wananchi kupata chakula na mazao ambayo wanaweza kuuza na kupata fedha kwa ajili ya kuinua vipato vyao

Kwa upande wa Serikali nayo imekuwa ikinufaika kwa namna moja au nyingine kwa maana ya kwamba wananchi wanapokuwa na uelewa na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali katika shamba hilo wanapata kipato ,hivyo kupunguza utegemezi kwa serikali lakini wanaweza kuchangia miradi ya maendeleo.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...