KUTOKANA na kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili kwa jamii hapa nchini ikiwemo matendo ya ubakaji na ushoga,Baraza kuu la waislamu Tanzania(Bakwata)limeanza kuzunguka nchi nzima kutoa elimu na kukemea matendo hayo kwa waumini wake na kuishi kwa kufuata mafundisho ya Dini.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Da’awa na Tabligh kutoka Baraza kuu la Waislamu Tanzania(Bakwata) Sheikh Arif Surya,wakati akizungumza na waumini wa Kiislam baada ya kukamilisha Ibada ya Ijitimai iliyoambatana na Dua maalum ya kuliombea Taifa katika msikiti Mkuu wa wilaya ya Tunduru.

Ibada hiyo imefanyika kwa siku tatu ambapo viongozi kutoka Baraza la Waislamu(Bakwata)wilaya ya Tunduru na Bakwata makao makuu wamezunguka katika vijiji mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu na mafundisho kwa waumini wao.


Shekhe Surya alisema,lengo la ibada hiyo ni muendelezo wa viongozi wa Dini ya Kiislam wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt Abubakar Zuber,kukemea matendo maovu yanayoanza kushamiri kwa kasi kubwa hapa nchini ambayo ni kinyume na mafundisho ya dini hiyo na maagizo ya MwenyeziMungu.

Shekhe Surya alisema,baadhi ya watu kutoka mataifa ya nje wanafanya jitihada kubwa zinazokwenda kinyume na maadili na mafundisho ya MwenyeziMungu kwa kuwafundisha watoto wa kiume kujiingiza kwenye ndoa za jinsia moja.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,ametoa wito kwa viongozi wa Dini,viongozi wa kimila na wazazi wilayani humo kutumia sehemu ya muda wao kuzungumza na watoto na vijana.

Alisema,hatua hiyo itasaidia sana kupunguzana na kukomesha vitendo vya ukiukaji wa maadili vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya watu hapa nchini.


Alisema,vijana wakifundishwa vizuri mila,desturi na kushika mafundisho ya dini na wakawa na hofu ya Mwenyezi Mungu maovu mengi ikiwemo ndoa za jinsia moja,ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia vitapungua kwa kiwango kikubwa hapa nchini.

Aliongeza kuwa,serikali itaendelea kushirikiana na Dini zote katika kujenga maadili mema kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla,hata hivyo amewaomba viongozi hao kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza vema mipango ya maendeleo katika nchi yetu.

Aidha,Mkuu wa wilaya ametumia nafasi hiyo kukemea vikali vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wa kike na kiume na kuhaidi kwamba serikali ya wilaya itahakikisha inaongeza nguvu katika kupambana na ukatili na kuimarisha ulinzi kwa watoto hao.

Amewakumbusha viongozi wa dini wilayani humo, kuendelea kukemea vitendo vyote vinavyoweza kuwagawa Watanzania ikiwemo tofauti za Dini kwa kuwa sisi sote ni wamoja na kuwapongeza viongozi hao kwa kuendelea kudumisha amani,umoja na mshikamano.


Mtatiro amewasa wazazi na walezi kuweka mifumo imara ya ulinzi kwa watoto kuanzia ngazi ya familia,mtaa,mashuleni na sehemu nyingine ili kulinda haki na ustawi wa watoto na kuwaepusha na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya watu wazima katika jamii.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Bakwata wilayani Tunduru Abdala Kawanga,ameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wa Dini hali iliyowezesha wilaya hiyo kuwa na utulivu na wananchi kupata muda wa kufanya shughuli zao za uzalishaji mali.

Amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kupeleka mbolea za bure kwa wakulima wa zao maarufu la korosho na kuhaidi waumini wa Kiislam wataendelea kumuunga mkono katika jitihada za kuleta maendeleo hapa nchini.

 
Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Bakwata wilaya ya Tunduru Sheikh Abdala Kawanga kushoto,akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro wa pili kuhoto kutoa salamu za serikali baada ya kukamilika kwa Ibada ya Ijitimai na dua maalum la kuliombea Taifa iliyofanyika katika msikiti mkuu wa wilaya hiyo mjini Tunduru.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...