Na Oscar Assenga,MKINGA
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman amekerwa na utekelezaji wa mradi wa Maji Wilayani Mkinga wenye thamani ya zaidi ya Shs Bil 3.1 huku akiumuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba kuutembelea mradi huo na kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa kutabainika ubadhilifu wowote .
Mradi huo unaosimamiwa na wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo(RUWASA) ambao umeonekana hauna ufanisi wala tija kwa wananchi zaidi elfu kumi wanaokabiliwa na adha ya maji Wilayani humo.
Mwenyekiti huyo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki akiwa Wilayani Mkinga katika mwendekezo wa ziara yake iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho pamoja na kukagua miradi ya maendeleo na kusema watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema ni lazima wanyooshane mapema hasa kwa wale watumishi wazembe ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wake na kupelekea kukipa chama chetu taabu wakati wa kampeni hivyo hawatakubaliana nao na wanaanza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maswali toka kwa wananchi.
Aidha alisema kitendo kinachofanywa na Mamlaka hiyo ya Maji Wilayani Mkinga cha kujenga Tank la maji kwa ajili ya kuyasambaza kwa wananchi bila ya kuwa na chanzo cha uhakika wa maji ni uchonganishi wa Rais na wananchi wake.
Alisema alitegemea kuona mradi huo wa ujenzi wa tank hilo la maji mbali ya utekelezaji wa miundombinu ya kupokea maji,kusafirisha na kusambaza maji hayo ungekwenda sambamba na ukarabati wa bwawa la maji la Gombero ambalo ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa huduma hiyo.
Aidha alisema kilichoonekana kwenye mradi mradi huo tanki maji lipo lakini hakuna uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo mwisho wa siku Serikali inamlipa mkandarasi pesa nyingi huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma hiyo.
Alisema Rais,Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanahangaika mchana na usiku kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo itakayowasaidia wananchi kuondokana na kero mbalimbali jambo la kusikitisha watendaji waliopewa dhamana hiyo hawatekelezi walichoagizwa.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya bwawa hilo Meneja wa RUWASA Wilayani Mkinga Thomas Kaijage (TM) alisema bwawa hilo linachangamoto na linahitaji kufanyiwa ukarabati ili liweze kutunza maji ya kutosha yatakayoweza kuhudumia Wananchi hao na kuongeza kuwa wanategemea kupata fedha kwa bajeti ya mwaka 2023/2024.
Kaijage alisema kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kazi ya ukarabati wa bwawa hilo zitafanywa na wakala wa uchimbaji wa mabwawa na visima (DDCA) baada ya usanifu kukamilika.
Aidha alisema mradi huo unaojengwa Wilayani humo unakwenda sambamba na ujenzi wa Tanki la maji litakaloweza kuhifadhi mita za ujazo 300,vituo 28 vya kuchotea maji,Ofisi ya Chombo Cha watoa huduma ngazi ya jamii(CBWSO),Machujio ya Maji(treatment Plant),uchimbaji na ulazaji wa mabomba na ufukuaji wa mitaro mita 48,000 na ukarabati wa Nyumba ya Pampu(pump house).
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkinga(CCM) Dastan Kitandula alisema Rais ameridhia kata ya Gombero Wilayani humo kuboreshewa miundombinu ya usambazaji wa maji na ujenzi wa tank ili kuweza kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na adha ya Maji Wilayani humo.
Aidha alisema upo mradi wa maboresho ya Bwawa la Gombero amabalo ndio chanzo kikuu cha maji utakaogharimu Shs Bil 4,na mradi mkubwa utakaotoa maji mto Zigi kuelekea Horohoro ambao utagharimu zaidi ya Shs Bil 34 na kuifanya Wilaya hiyo kuondokana na adha hiyo ya maji.
Ziara ya Mwenyekiti huyo itadumu kwa takriban siku 20 ambapo atatembelea Wilaya za Mkinga,Muheza,Korogwe Mji na Korogwe Vijijini na Wilayani Lushoto kama alivyoahidi kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa Tanga mara baada ya kuchaguliwa na kushika wadhifa huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...