Na Khadija Kalili Michuzi Tv
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Mobhare Matinyi, leo Agosti 06, 2023 ameungana na viongozi kadhaa kuhudhuriahafla ya ufungaji ndoa 70 iliyofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Al Hikma, Chang'ombe Wilayani Temeke Dar es Salaam.
Mheshimiwa Matinyi ambaye alikuwa pia akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametangaza kumpatia bwana harusi mmoja ambaye ni mlemavu wa miguu, Ally Kundi kiasi cha Sh. 200,000 kila mwezi kwa mwaka mzima zikiwa ni kwa ajili ya kumchangia mafuta ya Bajaj aliyozawadiwa kwa kushtukizwa na Taasisi ya Al Hikma iliyoandaa hafla hiyo.
Taasisi hiyo inayoongozwa na Sheikh Nurdìn Kishki imemzawadia Bajaj hiyo Kundi, maarufu zaidi kwa jina la Babu Ally, ili kumkomboa kiuchumi. Bajaj hiyo ina thamani ya shilingi milioni 9.8.
Awali mara tu baada ya kuipokea zawadi hiyo huku akitokwa machozi ya furaha, ameshangaa tena kusikia viongozi wanne waliohudhuria hafla hiyo akiwemo Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto, wakimpatia shilingi milioni mbili za gharama ya mafuta ya kuanzia biashara yake.
Babu Ally ambaye ni mkazi wa Mwembe Yanga Wilayani Temeke ni muendesha Bajaji Jijini Dar es Salaam kwa kupeleka hesabu za jioni kila siku kwa tajiri wake.
Hafla hiyo imehudhuriwa na waumini wa dini ya Kiislamu zaidi ya 500 wakiongozwa na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Hassan Zungu.
Mbali ya kutoa salamu za serikali, Mheshimiwa Matinyi pia amekabidhi zawadi kwa wadhamini watatu wa shughuli hiyo iliyofuatiwa na chakula cha mchana.
Kwa mujibu wa Sheikh Kishki, amesema hii ni mara ya kwanza kwa ndoa 70 katika dini ya kiislamu kufungwa hapa nchini kwa pamoja.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Mobhare Matinyi (kulia) na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto (kushoto), wakiteta jambo na mlemavu wa miguu, Ally Kundi (Babu Ally) mara baada ya mlemavu huyo kuzawadiwa Bajaj mpya na Taasisi ya Al-Hikma na kisha viongozi kadhaa kumchangia shilingi milioni tano za mafuta. Aidha, Mheshimiwa Matinyi ameahidi kumpatia sh. 200,000/- za mafuta kila mwezi kwa mwaka mzima.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Mobhare Matinyi akizungumza kwenye ibada hiyo ya ufungaji wa ndoa 70 za vijana iliyofanyika Chang'ombe Dar es Salaam ambapo ameahidi kumlipa mlemavu wa miguu kiasi cha Shilingi 200,000 kwa mwaka mzima.
Sehemu ya kundi la mabwana harusi 70 ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioalikwa kuhudhuria hafla ya kuwafungisha ndoa katika ukumbi wa Taasisi ya Al-Hikma, Chang'ombe, jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...