Mwananchi kutoka nchini Malawi Jane Chimuyaka aliyekuwa akisumbuliwa na magonjwa ya moyo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kuanzisha matibabu ya moyo nchini kusaidia wagonjwa wa moyo waliopo Tanzania na nchi za jirani.

Jane aligundulika kuwa na matatizo ya moyo kupitia kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalam wa afya wa JKCI nchini Malawi mwezi Mei mwaka huu katika hospitali ya Queen Elizabeth.

Jane amesema kupitia kambi hiyo tatizo la moyo alilokuwa nalo liliweza kuonekana na kupewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi, hivyo kufika kwake katika Taasisi hiyo kumemsaidia kupata matibabu kwa haraka, karibu na nchi yake na kupunguza gharama kama angekweenda kutibiwa nje ya Afrika.

“Nilipofanyiwa uchunguzi pale Hospitali ya Queen Elizabeth niligundulika kuwa na mapigo ya moyo ya chini ya asilimia 30 hivyo kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu ya kuwekewa kifaa kisaidizi cha moyo na kufanya mapigo yangu ya moyo kufikia asilimia 90”, ameeleza Jane.

Jane amesema baada ya kupatiwa matibabu sasa anaweza kutembea kwa haraka, kupanda na kushuka ngazi, pamoja na kukimbia vitu ambavyo alikuwa hawezi kuvifanya kabla ya kupatiwa matibabu hayo.

“JKCI ni hospitali nzuri sana, Serikali ya Malawi haina haja ya kupeleka wagonjwa nchi za mbali baadala yake wawalete hapa Tanzania katika Taasisi ya JKCI kwani gharama za matibabu ni za kawaida ambazo zilipelekea hata mimi kuja hapa”, ametoa rai Jane.

Aidha kuhusu matibabu hayo daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI, Dkt. Alex Joseph amesema katika Taasisi hiyo wamekuwa wakitoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa kuwahudumia wagonjwa wa ndani na wa kutoka nchi za nje hasa za Afrika.

Dkt. Alex amesema JKCI hupokea wagonjwa wengi kutoka nje ya Tanzania hiyo imetokana na uboreshwaji wa sekta ya afya Tanzania hasa katika huduma za kibingwa zikiwemo matibabu ya moyo, vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wabobezi hivyo kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kama dunia inavyotaka.

“Katika siku chache za hivi karibuni tumepokea mgonjwa kutoka nchini Malawi ambaye mapigo yake ya moyo yalikuwa chini sana na baada ya matibabu mapigo yake ya moyo yameimarika na kuondoa hali zote za kuumwa alizokuwa akipata kabla ya kupatiwa matibabu”, ameeleza Dkt. Alex.

Dkt. Alex ameshukuru serikali ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya afya na kuokoa maisha ya watanzania ambao hawana uwezo wa kwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu na kuiomba Serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika vifaa tiba vya kisasa na kusaidia wagonjwa waliopo nchi za jirani.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...