Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wake jijini Algiers, Algeria tarehe 2 Agosti 2023.
Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf, Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akihutubia kwenye ufunguzi wa Ubalozi huo Waziri Tax ameeleza kuwa Tanzania na Algeria zimejidhatiti kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa lengo la kukuza ushirikiano wenye maslahi kupitia sekta za kipaumbele.
‘’Ni imani yangu kuwa Ubalozi huu utaendelea kuwa kiunganishi kati ya serikali zetu kwa kutoa huduma za kidiplomasia, kuhudumia Watanzania” alisema Dkt. Tax
Naye Mhe. Attaf ameeleza kuwa ziara ya Waziri Tax imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kuzungumza masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.
‘’Balozi zetu zitaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ili nia ya dhati ya kuimarisha na kukuza uhusiano iweze kuleta tija zaidi na kuziwezesha nchi zetu kunufaika kiuchumi,’’ alisema Mhe. Attaf.
Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa hati 8 za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya.
Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.
=====================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria tarehe 2 Agosti 2023. |
Picha ya pamoja, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...