MIKOANI-Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb) amesema, Serikali inatekeleza jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inaweka mazingira bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na kutatua changamoto walizonazo.
Dkt. Kijaji amesema hayo Agosti 1, 2023 alipotembelea Kiwanda cha Magodoro cha TANFOAM kilichopo jijini Arusha kujionea shughuli za uzalishaji magodoro na kisikiliza changamoto walizonazo.
Amesema,wizara yake inatekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji ambapo msingi wake ni kuondoa majukumu yanayofanana kati ya taasisi ili kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.
Akiongea na uongozi wa kiwanda hicho, Dkt.Kijaji amezitaka taasisi kuacha kufanya majukumu yanayofanana na kuzitaka kushirikiana katika kuwahudumia wafanyabiashara na wawekezaji ili kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa TANFOAM, Bw.Mechack Jimmy ameishukuru Serikali kwa jitahada mbalimbali inazozifanya katika kutatua changamoto za wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwawekea mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Ziarani Tanztech
Katika hatua nyingine,Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Serikali ya Awamu ya Sita haiko tayari kuwakwamisha wafanyabiashara na wawekezaji kushindwa kufikia malengo yao bali itawasaidia kukua na kuendelea kibiashara.
Sambamba na kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto zao ili kuhakikisha ufanyaji biashara wao unakuwa na tija na manufaa kwa Taifa.
Amesema hayo Agosti 1, 2023 alipotembelea Kiwanda cha Kutengeneza Vishikwambi cha Tanztech kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujionea uzalishaji huo na kusikiliza changamoto zao.
Dkt.Kijaji amesema, ameridhishwa na uwekezaji huo ikiwa ni hatua ya kutatua changamoto ya matumizi ya Vishkwambi katika shule za awali na zile za sekondari ambapo vitasaidia kufundisha wanafunzi namna bora ya kutumia TEHAMA katika mitaala ya elimu.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda hicho cha Tanztech, Bw. Gurveer Hans amesema, kiwanda hicho kipo tayari kushirikiana na Serikali katika kutoa bidhaa hiyo mashuleni na kwa watu binafsi kwa bei nafuu.
Kambi BRELA
Mbali na hayo, aziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt.Ashatu Kijaji (Mb.) ameiagiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuweka kambi mkoani Arusha kwa lengo la kurasimisha wafanyabiashara wa kilimo ili wapate leseni,TIN na vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi.
Dkt.Kijaji ameyasema hayo Agosti 1, 2023 alipokutana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha kwa lengo la kusikiliza changamoto walizonazo na kuzitatua
Aidha,Dkt Kijaji amewaonya wafanyabiashara wazawa kuacha mara moja tabia ya kukata leseni na kuwauzia wageni wanaokuja nchini kununua mazao hadi mashambani badala ya kuyafuata kwenye masoko husika
Amesema, endapo wafanyabiashara wa mazao wakirasimishwa na kupata leseni zao wataweza kutambulika, idadi yao itajulikana ili kurahisisha jitihada za kuwakwamua kiuchumi wafanyabiashara na wakulima wanauza mazao ya nafaka mbalimbali nchini.
Waziri Kijaji pia amebainisha kuwa, Serikali iko mbioni kufuta vibali vya usafirishaji wa mazao vinavyokatwa kila mkoa badala yake kibali kiwe kimoja tu kilicholipiwa kila kitu ili kuwezesha wafanyabiashara wa mazao kubeba mizigo yao na kupelekea mahali husika bila kukata vibali kila Mkoa wanapopita.
Awali Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wadogo (Machinga), Bi. Amina Samson Njoka akiongea mbele ya Waziri Kijaji amesema, wafanyabiashara wadogo katika jiji hilo wamekuwa wakilalamika kuhusu tozo nyingi kutoka OSHA, Jeshi la Zimamoto, Idara ya Uhamiaji pamoja na Halimashauri ambazo zimekuwa kero na kuomba kiwa tozo hizo zitizwe zote mara moja.
Sekta binafsi
Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda na Bishara, Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji (Mb.) amesema, Serikali inahakikisha sekta binafsi inaendelea kukua na hakuna kiwanda chochote kitakachofungwa ili kuendelea kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa
Waziri Kijaji ameyasema hayo Agosti 1, 2023 alipotembelea Kiwanda cha A to Z kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji kiwandani hapo na kusikiliza na kitatua changamoto walizonazo.
Aidha,amewataka wafanyabiashara kuwa na ushirikiano na Serikali katika kutoa changamoto wanazozipata na watoe mapendekezo ya suluhisho za changamoto hizo kwa kuwa Serikali ipo tayari kuzishughulikia.
Kiwanda cha ngozi
Pia, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amekitaka Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kuongeza uzalishaji wa bidhaa ili ziweze kukidhi mahitaji ya soko la ndani na soko la nje.
Waziri Kijaji ameyasema hayo Agosti 2, 2023 alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kitatua changamoto zilipo kiwandani hapo.
Aidha, Dkt.Kijaji amesema bidhaa hizo kama viatu, mabegi na pochi zinazotengenezwa na kiwanda hicho kwa kitumia malighafi za ndani ya nchi zina asilimia 100 ya kukidhi vigezo vya kuingia katika Soko la Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Sukari
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) amewataka maafisa biashara wote nchini kukagua bei ya sukari duka kwa duka na atakayekutwa na bei zaidi ya shilingi 3,200 achukuliwe hatua za kisheria.
Waziri Kijaji ameyasema hayo Agosti 2, 2023 alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kujionea shughuli za uzalishaji na kisikiliza changamoto walizonazo.
Dkt.Kijaji amesema ni jukumu la maafisa biashara kutambua mfanyabiashara yeyote atakayeuza sukari juu ya bei kati ya shilingi 2,800 na 3,200 kumchukulia hatua.
Dkt.Kijaji amesisitiza kuwa, ni jukumu la Serikali kulinda bidhaa yoyote inayotengenezwa nchini na kufanya juhudi za kila namna ili kuweza kuwasaidia wawekezaji na wafanyabiashara kuwa na mazingira bora na wezeshi ili kukuza biashara zao na kiwa na tija.
Aidha, amesema bidhaa zinazotengenezwa nchini zinatakiwa kuwanufaisha wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na biashara yoyote inayofanyika nje ya nchi inatakiwa kuwa rasmi.
Vilevile amekipongeza Kiwanda cha kuzalisha Sukari cha TPC kwa kutoa ajira zaidi ya elfu 3,200 na jinsi kinavojihusisha na utoaji wa huduma kwa jamii inayokizunguka.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Utawala wa Kiwanda cha TPC, David Shiltu amewasihi watanzania kuwa na amani kwa kuwa sukari ipo sokoni ya kutosha na hakuna uhaba na uzalishaji unaendelea.
Kiwanda cha Vipuri
Aidha, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt.Ashatu Kijaji (Mb.) amesema, Serikali itahakikisha inakisaidia Kiwanda cha Kutengeneza Vipuri Kilimanjaro ( KMTC) kufikia malengo katika masoko.
Amesema, Serikali itafanya hivyo kwa kuwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuona uzalishaji wa ndani unafanyika kupitia chuma kinachozalishwa nchini.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Kijaji amesema hayo Agosti 2, 2023 alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Kilimanjaro kujionea shughuli zilipo pamoja na kisikiliza na kitatua changamoto zao.
Aidha, amewapongeza wafanyakazi wa kiwanda hicho na kuwataka kuwa waaminifu kwa kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuweka mazingira bora ya biashara ili kuvutia wawekezaji katika viwanda vitakavyotumia vipuri vinavyotengenezwa na kiwanda hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...