Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU)
imetembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na
kuzitaka Taasisi za Umma na Binafsi zinazo daiwa na kituo hicho kulipa
madeni yao ili Kituo hicho kiendeshe shughuli zake kwa ufanisi na kuunga
mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuvutia utalii wa
Mikutano Nchini.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita
Kawawa, (Mb.) alipotembelea AICC na kamati yake kujionea Kituo hicho
kinavyotekeleza majukumu yake na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo
inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC jijini Arusha.
Akizungumza
katika kikao na menejimenti ya AICC, Mhe. Kawawa amezitaka taasisi za
umma na zile za binafsi kuhakikisha zinalipa madeni wanayodaiwa na Kituo
hicho ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi.
“Tumemsikia
MD wa AICC, Bw. Mafuru akiongelea changamoto mbalimbali zinazoikabili
AICC kuwa ni pamoja na madeni ambayo taasisi za umma na za binafsi
zinadaiwa, naseme hivi, taasisi zote za umma na za binafsi zilipe madeni
ya AICC, ili kituo kiweze kujiendesha kwa ufanisini, kuunga mkono
harakati za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuvutia mikutano mikubwa nchini
na kutoa mchango stahiki kwa pato la taifa,” alisema Mhe. Kawawa.
Amesema
kwa AICC kufanya kazi kwa ufanisi ni lazima iondokane na hiyo
changamoto ya madeni kwani kulipwa kwa madeni hayo kutaiwezesha kufanya
kazi zake kwa tija na ufanisi na hivyo kupata matokeo chanya na
kupongeza uendeshaji wa miradi ya maendeleo inayoendeshwa na kituo hicho
jijini Arusha
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya
Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, (Mb.) ameishukuru Kamati ya NUU
kwa kutembelea AICC na kuitaka Bodi ya AICC kuhakikisha inashughulikia
changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo yakiwemo madeni ya
taasisi mbalimbali ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe.
Byabato amewataka AICC wapitie upya na kwa ukamilifu orodha ya madeni
wanayodai na kuangalia namna bora ya kukusanya madeni hayo,
kuwakumbusha kwa viambatisho na kuangalia mbinu mpya za namna ya kudai
madeni hayo ikiwa ni pamoja na kuangalia kama utoaji wa "offer" za
kulipa madeni hayo kama unaweza kusaidiwa kupunguzwa kwa madeni hayo.
“ Pitieni upya madeni yenu, angalieni njia za kulazimishana pia kama
itawezekana, muwe na mikakati mahususi ya wadeni na njia za kulipa
madeni, kuna madhara kwa madeni hayo kuendelea kuonekana katika vitabu
vyenu nadhani mnajua kuwa yanaweza sababisha mshindwe kukopesheka pale
mtakapotaka kufanya hivyo katika taasisi za kimataifa,” alisisitiza Mhe.
Byabato.
Awali akizungumza katika kikao na Kamati ya NUU,
Mkurugenzi Mtendaji wa AICC Bw. Ephraim Mafuru amesema AICC inaandaa
mkakati wa kipaumbele utakaoiwezesha AICC kutekeleza vipaumbele vyake
ili iende na wakati na kuhimili ushindani wa soko la Diplomasia ya
Mikutano.
Amesema AICC pamoja na kufanya shughuli zake katika
mazingira ya ushindani, inakabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwemo
madeni ya muda mrefu ambayo taasisi za serikali na za binafsi
hazijailipa AICC kwa muda mrefu sasa.
“Kwa sasa AICC inatekeleza
shughuli zake kwa kuitangaza nchi katika nyanja ya utalii wa mikutano
na matukio na hivyo kuvutia mikutano mingi kuja nchini kwa kuwa vituo
vya mikutano duniani hufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali na
wadau wengine ambao ni wanufaika wa moja kwa moja wageni wanapo kuja
nchini kwa ajili ya mikutano,” alisema Bw. Mafuru.
Amesema AICC
imeamua kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na kufanya mabadiliko
yanayoendana na wakati kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Kituo wa mwaka
2022/2023-2026/2027 ulioidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi mwezi Juni
2022 na kuanza kutumika rasmi mwezi Julai 2022.
Naye Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Saidi Shaib Mussa akizungumza katika kituo hicho ameipongeza Bodi
na Menejimenti ya AICC kwa kutokufanya kazi kwa mazoea na kuwaahidi
kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na kufanya nao kazi bega kwa bega
ili kufanikisha utendaji wao.
Kamati Hiyo pia imekagua miradi
mbalimbali ya uwekezaji ya nyumba za makazi, na hospitali na viwanja vya
Kituo hicho na kuonyesha kuridhishwa na usimamizi na uendeshaji wa
miradi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) akiwa na baadhi wa Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo walipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) walipotembelea kituo hicho jijini Arusha kujionea kinavyotekeleza majukumu yake na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa kwanza kulia) akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (wa pili kulia) na baadhi wa Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo wakiangalia ukumbi wa Simba uliopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) walipotembelea kituo hicho jijini Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru akiwaelezea Waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) walipotembelea majumba ya Kituo hicho yaliyopo eneo la uzunguni jijini Arusha walipotembelea kituo hicho na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru alipowaelezea Waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, katika picha kushoto ni Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia mausala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AICC Balozi Begam Taj wakati wajumbe ya Kamati hiyo walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) akimsikiliza mmoja wa Wabunge na mjumbe wa kamati hiyo akiuliza swali kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru wakati wajumbe ya Kamati hiyo walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa kwanza kulia) akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kushoto) wakimsiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru hayupo pichani wakati Kamati hiyo ilipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AICC Balozi Begam Taj akizungumza kuwakaribisha Wajumbe wa Kamatiya NUU walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Wajumbe wa Kamati ya NUU wakiangalia moja ya kumbi za Mikutano katika Kituo cha AICC walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya NUU wakifatilia majadilianookati ya Kamati ya NUU na Menejimenti ya AICC wakati Kamati ya Bunge ya NUU ilipotembelea Kituo hicho jijini Arusha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...