Na Mwandishi Wetu

GEITA Gold Mining Limited (GGML) imeibuka kuwa kampuni inayoaminika zaidi kwenye sekta ya madini katika tuzo za mlaji (Consumer’s Choice Awards Africa) zilizotolewa mwisho mwa wiki iliyopita.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo zilizofanyika jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa GGML, Stephen Mhando alisema, "Tuzo hii ni uthibitisho wa kazi bora na muhimu tunayoifanya nchi nzima. Moja ya maadili yetu ya msingi ni kuhakikisha kuwa jamii inanufaika kutokana na uwepo wa GGML katika eneo hilo.

Amesema kampuni hiyo ambayo vipaumbele vyake vinalenga kuzingatia utu na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yake, vimeendelea kuimarisha mahusiano mazuri baina ya kampuni hiyo kupitia mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Awali, akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo hizo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema Serikali inatambua maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na Serikali pekee bali kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambayo ni chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi na hivyo Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Dk. Biteko alimwakilisha Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo ya utoaji wa Tuzo za Mlaji (Consumer’s Choice Awards Africa) amesema kutolewa kwa tuzo hizo ni kielelezo cha mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora ya kibiashara hapa nchini.

“Hivyo wawekezaji wenye mitaji tunawakaribisha mje muwekeze Tanzania na tunawaahidi kwamba Serikali itawapa ushirikiano ili fedha mnazoweka kwenye biashara ziwape faida na pia Tanzania ifaidike kwa uwepo wa miradi husika,” amesema Dk.Biteko

Amesema tuzo hizo zilizoanza mwaka 2019 zinahusisha walaji na watumiaji wa bidhaa ambao hutoa maoni na hupiga kura kuchagua kuridhishwa kwao kwa huduma wanazopata kutoka kwa watoa huduma na kueleza kuwa amefurahishwa na namna upigaji wa kura unavyofanyika kwani wale tu wanaotoa huduma bora ndio wanapata nafasi ya kupigiwa kura na kupewa tuzo.

Dk. Biteko amewapongeza waandaaji wa Tuzo hizo ambazo sasa zinafanyika kwa mwaka wa Tano. Pia amepongeza washindi wote kwa kutoa huduma bora na kuzalisha bidhaa bora.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amesema tuzo hizo ni muhimu kwani zinakumbusha umuhimu wa wazalishaji, watoa huduma na wafanyabiashara kumjali yule anayepokea bidhaa yao au huduma yao.

Ameongeza tuzo hizo zimechangia katika uboreshaji wa utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazoenda sokoni hivyo amewapongeza waandaaji wa Tuzo hizo ambazo sasa zimefikia mwaka wa Tano huku wigo wake ukiongezeka kutoka ndani ya Tanzania pekee na sasa ni Afrika kwa ujumla.

Tuzo za Consumer’s Choice Awards zimeandaliwa na kampuni ya Lavine International Agency na kampuni ya Choice Awards Africa ambapo muanzilishi wa Tuzo hizo ni Diane Laizer.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...