NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WASWAHILI wanasema 'Asiye na Mwana abebe Jiwe, na wazaramo wanausemi wao ule 'Kidela mwali kivika', misemo hii inatupa picha kamili kwasasa jamii kila mmoja kufanya maamuzi sasa katika kujitokeza kupima, Virusi Vya Ukimwi, jambo ambalo limekuwa gumu kwa baadhi ya watu.

Katika hali ya kawaida kuna baadhi ya watu wamekuwa ni wagumu kujitokeza kuangalia afya zao hasa katika suala la kupima Virusi vya UKIMWI mara kwa mara, hii inachangizwa na ukosefu wa elimu kwa baadhi ya jamii kuhusu umuhimu wa kujua afya zako (kujitokeza kupima).

Kupima VVU inasaidia kufahamu ni watu wangapi wameambukizwa ama wanaishi na VVU ili kuweza kupata takwimu sahihi na kuona ni namna gani tunaweza kupunguza ama kuzuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi.

Kipindi cha nyuma hasa miaka ya 2000 hadi 2010 jamii ambayo ilikuwa inaishi na Virusi Vya Ukimwi ilikuwa inapata shida hasa kunyanyapaliwa pindi wanapogundulika na Virusi hivyo kwani wengi walikuwa hawajaelewa kwa undani zaidi kuhusu maambukizi hayo.

Lakini katika kipindi hicho mpaka sasa Serikali kupitia taasisi zake ikiwemo Tume ya Kudhibiti Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha wanashirikiana na jamii katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU hasa kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa njia mbalimbali kuhusu masuala ya UKIMWI na matokeo yake yamekuwa yakiridhisha siku hadi siku hasa kwa takwimu ambazo wamekuwa wakizitoa TACAIDS.

Imeelezwa kuwa, Tanzania imepunguza maambukizi ya UKIMWI kwa asilimia themanini na nane (88%) kutokana na vifo vitokanavyo na UKIMWI kupungua kwa  asilimia hamsini   (50%) kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.

Hii inaamana kwamba jitihada ambazo zinafanyika kupitia vyombo husika inaleta hali ambayo inaridhisha hasa katika kuhakikisha tunapunguza ama kuondoa kabisa maambukizi mapya ya VVU nchini.

Hivi karibuni katika mawasilisho yaliyohusu tathmini ya hali ya UKIMWI nchini katika semina ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI kuhusu majukumu ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania yaliyofanyika Mwezi Aprili, 2023 Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ufatiliaji na Tathmini TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela, alisema tafiti  zinaonesha kuwa, Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima miaka 15 na zaidi yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020 na Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Mother to child transmission) yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.

Sambamba na hali hiyo, Dkt. Jerome alisema kuwa Serikali inatakiwa kuongeza nguvu katika eneo la kuzuia maambukizi mapya ya VVU  hasa kwa Vijana kwani zaidi ya theluthi  moja ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24, hususan vijana wa kike.

Tukiachana na hali ya kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU, je suala la kuwafuatilia watumiaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV) limefikia wapi, kwani ni njia rahisi kufahamu takwimu kamili ya watu ambao wana Virusi Vya Ukimwi na kuona ni namna gani wanaweza kuzuia maambukizi mapya kujitokeza.

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa kwa mwaka huu yanatarajiwa kufanyika Mkoani Morogoro katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro Disemba 01,2023, ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Katika Maadhimisho hayo, yenye kauli mbiu isemayo "jamii iongoze Kutokomeza UKIMWI" itaweza kutusaidia tukapata picha kamili kuhusu hali ya sasa ikoje kuanzia idadi kamili iliyopo ya watu waishio na VVU, idadi ya Vifo pamoja na hali ya maambukizi mapya ikoje, hii itaweza kusaidia jamii kufumbuliwa macho na kuweza kuendelea na kujikinga na maambukizi mapya.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...