Na. Peter Haule, WF, MwanzaMakongamano ya Kodi yanayofanywa na Wizara ya Fedha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida yamewezesha kufanyiwa maboresho kwa zaidi ya maeneo 57 ya kikodi katika mwaka wa Fedha 2023/2024 huku hatua hiyo ikilenga kusisimua ufanyaji biashara, kulinda viwanda vya ndani na kuchochea uwekezaji nchini.Hayo yamesemwa Jijini Mwanza na Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, wakati timu ya watalaam wa masuala ya fedha na uchumi wa Wizara ya Fedha ilipokusanya maoni ya kuboresha kodi kwa ajili ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.Alisema kuwa kuanzishwa kwa Kongamano hilo kumeleta tija katika maboresho ya mfumo wa kodi ambapo katika maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2023/24 ushirikishwaji wa wadau uliongezeka.“Maoni yaliyotolewa yalisaidia kufanya maboresho kwenye maeneo 57 ambapo malengo yake ni pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia uwekezaji nchini na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani”, alieleza Bw. Mhoja.Bw. Mhoja aliyataja baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa kazi kuwa ni pamoja na kuongeza kima cha usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka shilingi milioni 100 hadi milioni 200.Maeneo mengini ni kuanzisha utaratibu wa kufanya marekebisho kwenye viwango vya ushuru wa bidhaa kila baada ya miaka mitatu kwa ajili ya utulivu wa kisera, kusamehe VAT ya uuzaji, uingizaji na ukodishwaji wa ndege ikiwa ni pamoja na matengenezo ya ndege.Pia alisema kuwa Serikali imeondoa VAT kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza vifungashio vya madawa na kuondoa ada ya ukaguzi kwenye madini yanayouzwa kwenye vituo vya kusafishia madini nchini.Bw. Mhoja alisema kuwa lengo la makongamano hayo yatakayofanyika maeneo mbalimbali nchini ni kuboresha uratibu wa ukusanyaji maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ili kuborsha Sera za utozaji Kodi hatua itakayochochea ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na ya kimkakati halikadhalika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Aidha amewashukuru wananchi wa mkoa wa Mwanza kwa kuitikia wito na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kuhusu kodi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, alisema timu ya wataalamu wenye weledi wa kutosha imeyachukua maoni hayo ili kuweza kuyafanyia kazi.Kwa upande wake Mwenyekiti Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo mkoa wa Mwanza (TCCIA) Gabriel Kenene, ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuamua kuwafuata wananchi ili kuweza kupata maoni yao ikiwa pia ni shauku ya wabunge walio wengi.Ameiomba Wizara ya Fedha kuendelea kufanya makongamano kama hayo ili kuwasikiliza wananchi na kujionea hali halisi ya mazingira yao ya biashara ili Sera zinazotungwa ziwe rafiki kwa wananchi.Makongamano ya kodi Kitaifa yanayofanyika kikanda yanaendelea na lengo ni kukusanya maoni ya kodi kwa ajili ya kuboresha Sera za Utozaji kodi kwa mwaka 2024/25.Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, akieleza kuhusu umuhimu wa maoni ya wananchi katika kuboresha Kodi, wakati wa Kongamano la Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi. Kulia ni Afisa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza, Bw. Giliard Nguve na kushoto ni Mwenyekiti Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo mkoa wa Mwanza (TCCIA) Bw. Gabriel Kenene.Katibu Mtendaji wa Viwanda vya Samaki Mkoa wa Mwanza, Bw. Onesmo Sulle, akitoa maoni ya Kodi kuhusu sekta ya Viwanda vya Samaki wakati wa Kongamano la Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi.Mkurugenzi wa wazalishaji wa Mvinyo Mkoani Mwanza, Bw. Leopord Lema, akiipongeza Serikali kwa maboresho ya kodi kwenye vinywaji vikali na kupendekeza kuendelea kwa maboresho hayo wakati wa Kongamano la Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi.Meneja wa kiwanda cha kutengeneza nyavu za kuvulia dagaa (Ziwa Met Ltd), Bi. Gift Christopher, akieleza namna ya kuboresha kodi ili kurahisisha uvuvi endelevu wa dagaa, wakati wa Kongamano la Kodi Kikanda lililofanyika jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi.


Mzee Abubakar Hassan Self Mkazi wa Mwanza, akitoa maoni yake kwa Timu ya Wataalamu wa Sera za Kodi waliofika Mkoani Mwanza kukusanya maoni kwa lengo la kuboresha kodi ikiwa ni mwendelezo wa Makongamano ya Kodi Kikanda.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mwanza)Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...