Na. Damian Kunambi, Njombe

Kufuatia changamoto wanazozipata wakazi wa kata ya Ibumu iliyopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe pamoja na wakazi wa kata ya Litumbandyosi iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ya kusafiri kwa kutumia mitumbwi katika mto Ruhuhu na kupelekea baadhi yao kuliwa na mamba waliopo katika mto huo unaotenganisha wilaya na mikoa hiyo serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 2.9 kwaajili ya mradi wa ujenzi wa daraja Igugu.

Mradi huo umetambulishwa rasmi kwa kufanya hafla fupi iliyohuzuliwa na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga na mbunge wa jimbo la Mbinga Benaya Kapinga,  diwani wa kata ya Ibumi Edward Haule, Diwani kata ya Litumbandyosi Prisca Haule, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wahandisi wa wilaya zote mbili pamoja na wananchi wa kata ya Ibumi na Litumbandyosi.

 Akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa Mamlaka ya barabara mijini na vijijini (TARURA) Mhandisi Butene Jilala amesema  mradi huo tayari umekwisha anza kwa kuifungua barabara yenye urefu wa km. 20 ambayo itawezesha kusafirisha vifaa mpaka katika eneo la mto huo ambapo mpaka sasa barabara hiyo km. 17 zimekwisha tengenezwa na kusalia km. 3 pekee.

Ameongeza kuwa daraja hilo litakuwa na njia mbili za magari na njia moja ya watembea kwa miguu huku upana wake ukiwa ni  Mita 9 urefu Mita 65 na litakuwa na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa hadi tani 120 hivyo  mkandarasi wa kujenga daraja hilo tayari amepatikana na litajengwa kwa kipindi cha miezi sita.

 " Hili daraja  litakuwa kubwa sana na litadumu kwa miaka 100 ijayo kwani tutalijenga kwa nguzo nne ambazo ni imara ambapo nguzo mbili ambazo ndio nguzo mama zitajengwa moja upande wa Ibumi na nyingine Litumbandyosi na nguzo mbili zitajengwa katikati ya mto". Amesema Mhandisi Jilala.

Aidha kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga Mhandisi Osca Mussa amesema daraja hilo lina manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili hivyo katika kushirikiana kukamilisha ujenzi huo na wao wameanza kuifungua barabara itakayofika katika eneo la mto huo kwani pasipo kuifungua barabara hiyo ujenzi wa mradi huo unaweza kukwama kwakuwa baadhi ya vifaa vya ujenzi vinatakiwa kupitia wilayani Mbinga.

Hata hivyo kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema daraja hilo lina umuhimu sana kwa wananchi kwani wananchi wake wanajishughulisha na kilimo biashara  cha mazao mbalimbali kama mpunga, mahindi na maharage na soko lao kubwa lipo katika upande wa Wilaya ya Mbinga hivyo kutokana na umuhimu huo aliona haja ya kutafuta fedha za ujenzi wa daraja hilo.

Sanjali na hilo ameongeza kuwa mkoani Ruvuma kuna hospitali kubwa ya Peramiho ambayo wakazi wengi wa Ludewa hufika kupata huduma, lakini waendapo huwalazimu kusafiri umbali wa zaidi ya km. 408 hivyo daraja hilo litakapokamilika litasaidia watu kwenda kupata huduma hizo kwa kusafiri umbali wa km. 140 pekee.

" Ndugu zangu nimeshirikiana vyema na mbunge mwenzangu wa Mbinga katika kuwasilisha changamoto hii ya wananchi wetu na tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aliona umuhimu wa jambo hili na kutupatia kiasi hiki cha fedha ili kuwaondolea wananchi kikwazo hiki kinachozuia kukua kwa uchumi wao na kupata huduma za msingi". Amesema Kamonga.

Naye mbunge wa Jimbo la Mbinga Benaya Kapinga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakomboa wananchi hao kwani hatua hiyo inakwenda kubadilisha historia ya wananchi na kukuza uchumi wao.

 Edward Haule ni Diwani wa kata ya Ibumi ambaye ndiye aliyetoa wazo la kuunganisha kata hizo kwa kujenga daraja miaka 23 iliyopita lakini katika kipindi chote hicho wazo lake hilo halikuweza kutekelezwa hivyo amefurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa na kuipongeza serikali huku wananchi nao wakionyesha furaha zao.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...