Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amefungua Tamasha la Utalii
"Chato Utalii Festival 2023" linalofanyika wilayani Chato, mkoani Geita
kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii na kutangaza fursa
mbalimbali za uwekezaji zilizopo mkoani humo.
Akizungumza wakati
akifungua tamasha hilo Novemba 26, 2023 ambalo linaambatana na maonesho
mbalimbali ya fursa zilizopo mkoani humo, alisema tamasha hilo limebeba
dhana mbalimbali za uwekezaji hasa kwa upande wa kilimo, mifugo na
uvuvi, utalii, utamaduni na michezo.
Alisema fursa za uwekezaji
zilizopo katika Wilaya ya Chato ni nyingi huku akiwahimiza wananchi na
wawekezaji mbalimbali kuzitumia ili ziweze kuwaletea ufanisi na kukuza
uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Aidha, Waziri Ulega alitumia
fursa hiyo kutaja maeneo mbalimbali ambayo yana fursa za uwekezaji
mkoani humo huku akibainisha kuwa katika sekta ya uvuvi pekee Mhe. Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili
ya kujenga mwalo na soko kubwa la kisasa la samaki wilayani chato
ambalo litatoa fursa za kibiashara na uongezaji thamani wa mazao ya
samaki na dagaa.
Halikadhalika, aliongeza kwa kusema kuwa Mhe.
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa takriban shilingi Bilioni 1.8 kwa
ajili ya kufanya ujenzi wa kituo kikubwa cha kuzalisha vifaranga vya
samaki cha Rubambagwe kilichopo wilayani Chato ambacho kitawezesha
wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika ukanda wa Ziwa Viktoria
kuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora vya samaki.
Kwa upande
wa sekta ya mifugo, Waziri Ulega alisema Wizara imejenga mnada wa mifugo
wa kisasa wa Buzirayombo ambao unatoa fursa kwa wafugaji kufanya
biashara zao za mifugo kisasa huku akifafanua kuwa kufuatia uwepo wa
idadi nzuri ya mifugo kunatoa fursa nyingine ya kujenga kiwanda cha
kuchakata nyama.
Fursa nyingine alizozibainisha Waziri Ulega ni
pamoja ujenzi wa hoteli kubwa za hadhi ya nyota tatu hadi tano kwa kuwa
viwanja vinapatikana katika wilaya ya Chato, Kilimo cha umwagiliaji kwa
kuwa sehemu kubwa ya wilaya ya Chato imezungukwa na maji ya Ziwa
Victoria na ujenzi wa viwanda vya Nguo kutokana na kuwepo kwa kinu cha
kuchambulia pamba.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kulia) akiwa na Mkuu
wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella (katikati) na viongozi
mbalimbali mkoani humo muda mfupi baada ya kufungua Tamasha la Utalii "
Chato Utalii Festival 2023" linalofanyika wilayani Chato, mkoani Geita
Novemba 26, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega akimkabidhi mmoja wa washindi wa mbio za baiskeli
katika Tamasha la Utalii " Chato Utalii Festival 2023" linalofanyika
wilayani Chato, mkoani Geita Novemba 26, 2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...