Na Said Mwishehe, Michuzi TV
KATIKA kuadhimisha Kampeni ya siku 16 za Kupinga ukatili wa Kijinsia nchini, Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kwa niaba ya Mtandao wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia(MKUKI)wameiomba Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kufanya kazi masuala mbalimbali yakiwemo ya kuomba Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kutunga sheria mahususi ya kushughulikia masuala ya Ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo kama ilivyoanishwa na Sheria ya mfano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Model Law) ambayo Tanzania ni Wanachama na tulishiriki katika kuitengeneza.
Maombi hayo yametolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa WiLDAF Dk.Monica Mhoja mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dk.Dortoth Gwajima aliyekuwa amemwakilisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho hayo yaliyoshirikisha makundi ya wadau mbalimbali nchini wakiwemo wiLDAF na MKUKI ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsi nchini
Ametaja maombi mengine ni wanaiomba Serikali kupitia Wizara yenye dhamana kuharakisha mchakato wautungaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili waKijinsia (MTAKUWA II), pia Serikali iwekeze bajeti ya kutosha itakayosaidia kamati zilizoundwa katika utekelezaji wa MTAKUWA kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha wameiomba Serikali kufanya mapitio ya kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa na uchakataji wa Takwimu za Ukatili wa Kijinsia ili ziweze kuoana kati ya watoa huduma hizo. Kwa hali ilivyo sasa mifumo ya watoa huduma wakiwemo Polisi, Ustawi wa Jamii, Afya, Mahakama nk haifanani na hivyo kusababisha mashauri mengi yamekuwa yakiendelea kwa kukosa ufumbuzi yakinifu.
Maombi yao mengine kwa Serikali ni Kuharakisha wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1972 kwani Sheria hiyo imewapa nguvu wanaume na familia kutumia mapungufu yaliyopo kama fursa kuwaozesha watoto na kupenya mkono wa sheria.Sheria hiyo imedogosha sheria zingine kama vile Sheria ya Elimu na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
“Ucheleweshaji wa mabadiliko ya sheria hii, umeendelea kusababisha watoto wakike kuolewa katika umri mdogo na kukumbana na ukatili wa kijinsia kwa sababu ya kushindwa kuhimili mikiki ya ndoa,Tunatambua kwamba Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ipo kwenye mchakato wa kukusanya maoni ya wadau juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa.
“Hata hivyo, mchakato huu umechukua muda mrefu kufuatia maamuzi ya kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Z.Gyumi (Rufaa ya Madai Na. 204 ya mwaka 2017, Mahakama ya Rufani ya Tanzania Jijini Dar es Salaam), katika hukumu yake iliyotolewa Oktoba 15,2019 ilikiona kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa [Sura ya 29 ya Sheria za Tanzania, 2022] kuwa kinyume cha katiba na kuiamuru serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ndani ya mwaka mmoja. Hata hivyo mpaka sasa, Sheria hii bado haijafanyiwa mabadiliko.Tunaomba Serikali iharakishe mchakato ili wasichana na watoto wetu wakike waweze kulindwa na sheria,”amesema.
Wakati ombi lao la tano kwa Serikali kupitia Wizara yenye dhamana kuimarisha Mwongozo na kuweka kanuni madhubuti zitakazo linda Wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji kwenye siasa wakati wa uchaguzi ili waweze kushiriki kikamilifu katika michakato yote ya kidemokrasia ikiwemo uchaguzi.
Akiendelea kuzungumza kwenye maadhimisho hayo Dk.Mhoja amesema wanaendelea kutoa shukrani zao za dhati kwa Rais Dk.Samia kwa uhodari na uongozi mahiri katika kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, watoto na wote wanaopitia vitendo hivyo katika jamii, kwa hakika umekuwa kielelezo bora katika harakati hizo.
“Sisi wana MKUKI tupo tayari na tunaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kuwa na jamii salamayenye kuchochea maendeleo endelevu. Wana MKUKI tuko pamoja nawe, tunakutakia hekima na busara na kila la kheri katika kazi zako. Tunatambua na kuthamini jitihada zake za kuwainua wanawake nchini. Sisi wana MKUKI tunakupenda na tutaendelea kukuunga mkono.
Kwa upande wake Waziri Dk.Gwajima ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuchukua katika kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa kijinsia nchini vinakomeshwa huku akisisitiza umuhimu wa jamii kwa makundi yote yakiwemo ya wanaume kushiriki kikamilifu kukomesha vitendo hivyo huku akisisitiza yote ambayo yameelezwa na WiLDAF na MKUKI pamoja na wadau wote wiraza yake itafanyia kazi na mengine yatakayokuwa juu ya uwezo wao atayafakisha kwa Rais kwa hatua na maelekezo.
“Nimepokea hoja zote ,tutazichambua lakini kwanza kwa kukaa na mawaziri wa kisekta na nyingie tutazichambua kwenye Wizara yetu kabla ya kupeleka kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ili ajue hoja zenu .Mmezungumza kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya ndoto, sheria zinazosimamia chaguzi na siasa.
“Kabla ya kumpelekea Rais niseme mwenyewe hapa Wizara yangu ni wizara mtambuka , hivyo tutaratibu sekta nyingine zote kutekeleza yale ambayo tunaona yatasaidia safari yetu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.Tutakwenda kujadili kwa mfano sheria ya elimu na sheria ya ndoa zinakwenda tofauti.Hivyo tutafuatilia na hatimaye kutoa taarifa rasmi ya mchakato wa sheria hizo ulikofikia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Doroth Gwajima akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho wa Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...