Na Mwandishi Wetu

DAKTARI Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI), Joel Mwinza (44), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam jinsi alivyomtibu Deogratus Minja aliyedaiwa kushambuliwa na nyundo na mfanyakazi wa benki , Ibrahim Masahi hadi kusababishia kushonywa nyuzi kichwani.

Aidha, amedai kuwa alipompokea Minja alikuwa na majeraha kichwani, mgongoni, mkononi na pia kuna sehemu alikuwa amechanika kisogoni, kwa hiyo alitumia mashine ya X-ray na CT Scan kumchunguza mwili wake.

Dk Mwinza amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya Masahi anayetuhumiwa kumshambulia kwa nyundo Minja Januari 11,2023 eneo la Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam.

Amedai kuwa Januari 24,2023 alimpokea mgonjwa anaitwa Deogratus ambaye alipelekwa kwake na daktari kutoka Kitengo cha dharula cha wagonjwa MOI akiwa na historia ya kujeruhiwa na jirani yake, alimleta ili amtibu shida yake ya mifupa.

"Alikuwa ana majeraha kichwani, mgongoni, mkononi, alikuwa amechanika kichwani ameshonwa nyuzi na pia bega la kulia lilikuwa na maumivu, nilimfanyia vipimo, X-ray ilionesha amevunjika bega na CT Scan ilionesha ameumia kwenye ubongo," Amedai Dk Mwinza

Amedai kuwa baada ya vipimo, akaanza kumpatia matibabu, kwa kumuandikia dawa na katika tatizo la bega alimpa kifaa tiba ambacho alikitumia kwa muda wa wiki sita na kwa upande wa majeraha yaliyoshonwa yalisafishwa na kutolewa nyuzi.

" Mgongwa alinipa fomu ya polisi Pf3 nikaijaza, nikampangia siku kwamba baada ya wiki mbili arudi tena MOI kwa ajili ya uchunguzi. Sikumbuki tarehe, lakini nakumbuka niliitwa na uongozi ili nitoe ushirikiano kwa polisi kuhusiana na mlolongo wa matibabu niliyompa Deogratus," Amedai.

Dk Mwinza aliendelea kudai kuwa daktari mwenzake alimpokea Minja Januari 12,2023, alikuwa amepewa rufaa kutoka Hospitali ya Bochi, baada ya kudai hayo aliiomba mahakama ipokee fomu hiyo kama kielelezo katika kesi hiyo, ambapo mahakama ilikipokea kwa sababu Wakili wa utetezi, Nestory Wandiba hakuwa na pingamizi.

Katika ushahidi wake, Minja amedai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alimkuta kijana wa jirani huyo, baada ya kumuona alizungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa ambae yeye hakuielewa.

"Ghafla kijana alikuja mbele yangu akanizuia nisipite, mara geti likafunguliwa akatoka Masahi akanihoji kwamba mimi ni kama nani na kwenda kumshitaki Serikali za Mitaa, sikumjibu chochote kijana wake akanipiga ngumi,"

"Nilimgeukia jirani yangu ili amuonye kijana wake, lakini na yeye aliinua shati lake akatoa nyundo akanipiga nayo kichwani baada ya kupata maumivu makali nilianza kukimbia huku nikipiga kelele za kuomba msaada,"amedai Minja.

Amedai kuwa, alianguka chini ndipo Masahi akaanza tena kumshambulia na nyundo mgongoni, maumivu yalipomzidi aligeuka, akampiga na nyundo kwenye mkono wa kulia na kwenye bega. Jirani mmoja alifungua geti na kumsaidia kwa sababu alikuwa ana kuja damu nyingi walimpeleka Hospitali ya Bochi kwa matibabu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...