Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

WAZIRI wa Elimu ,Prof.Adolf Mkenda ametoa rai kwa walimu wakuu nchini kuwa makini na mashirika binafsi , Taasisi zisizo za Kiserikali zinazokwenda kwenye shule zao kutoa misaada ikiwemo miswaki, vidonge kwa wanafunzi ili kuondokana na sintofahamu za misaada hiyo.

Aidha amewataka Wakurugenzi wa halmashauri kutoa fursa za ruksa kwa walimu ambao wanahitaji kwenda kujiendeleza kitaaluma pasipo kuwawekea vikwazo.

Prof.Mkenda alitoa rai hiyo kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Cha Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM ) Bagamoyo Mkoani Pwani kwa minajili ya kutunuku stashahada ya Uongozi na usimamizi wa elimu, stashahada ya uthibiti ubora wa shule na Astashahada ya Uongozi usimamizi na utawala wa elimu kwa wahitimu wapatao 920.

Alihimiza umakini kwa wanafunzi mashuleni ,kwani ualimu ni kazi kubwa na wana wajibu wa kusimamia watoto.

"Kuna wajibu ambao hawawezi kuukwepa ,kuna shule moja iliyopo Mkoani Pwani ambapo kuna wazungu walienda na kutoa zawadi ya miswaki na vidonge vyenye rangi rangi kwa wanafunzi, havijulikani vidonge vya nini ,wazazi walihoji wengine walikuja juu kutaka kujua vidonge ni vya nini wakati watoto wao hawaumwi"

"Nilifikishiwa taarifa kuwa wanafunzi wamepokea zawadi ya miswaki na vidonge hivyo ambavyo hatujui vinafanya nini ama kushawishi vitendo gani ,Nilipouliza nikapata majibu kuwa ugeni huo ni kawaida maana ni awamu ya pili wameshaenda kutoa vitu hivyo kwa wanafunzi shuleni hapo, sasa tunajuaje zina madhara gani "alieleza Prof Mkenda.

Prof.Mkenda alisema aliagiza wadhibiti ubora wafike kufuatilia suala hilo na hatua na utaratibu unaotakiwa zimechukuliwa .

Aliomba walimu kuzidisha uangalifu, sambamba na kudhibiti misaada inayofika kwenye maeneo yao ,na wawe wasimamizi wakubwa ili kuepusha madhara ya baadae kwa watoto.

Hata hivyo alipongeza kazi kubwa inayofanywa na walimu nchini na kuwataka waongeze juhudi ili kuinua taaluma .

Pamoja na hayo aliwaasa Wakurugenzi wa halmashauri kutoa ruksa na kuwapa fursa walimu wanaohitaji kujiendeleza kitaaluma .

Prof Mkenda alisema licha ya Rai na wito wake kwa walimu , Serikali inaendelea na jitihada kubwa kuboresha mazingira katika sekta ya elimu na kuwekeza bejeti kubwa .

"Kwasasa Serikali imeanza na maboresho ya sera na mitaala ya mwaka 2014 ,kwa kuja na mtaala mpya 2023 ,mchakato umemalizika ,sasa tunakwenda kwenye utekelezaji wake 2024"Alifafanua Mkenda.

Sanjali na hayo, Serikali inasimamiwa sera ,sheria, mitaala , idadi na ongezeko la walimu, wakufunzi,wahadhiri , kusimamia ubora wa walimu , vitendea kazi ikiwemo kwa wanafunzi wa makundi maalum na kuboresha miundombinu kwa kuongeza majengo ya madarasa.

Awali Mtendaji Mkuu ADEM , Dkt. Siston Masanja alieleza waliotunukiwa vyeti ni kozi ya DELMA kutoka kampas za Bagamoyo,Mwanza na Mbeya 702 ,DSPA 214 sawa na asilimia 96.4 ,SELMA watatu.

Alieleza, wamepokea mageuzi ya mabadiliko ya Serikali kuhusiana na mtaala mpya na watausimamia kikamilifu kwa matokeo chanya.

Dkt Msanja alisema ,wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti ,lakini wanaendelea na ukarabati wa majengo katika kampas ya Bagamoyo.

"Tunafanya ukarabati wa majengo ya kampas ya Bagamoyo, na kampas ya Mbeya ambapo watakamilisha mwishoni mwa mwaka huu".

Rais mstaafu wa wanafunzi Evan Silinu alieleza watahakikisha wanatumia taaluma waliyoipata vizuri ,kwa kulinda raslimali za shule na kuwa na Uongozi ulio bora.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...