Na Joanita Joseph -TMC Habari

HALMASHAURI ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya Kongamano la fursa za uwekezaji mahsusi kwa ajili ya kuwafamisha wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo uwepo wa fursa mbalimbali za kiuwekezaji zilizopo Temeke

Kongamano hilo pia limetumika kutoa elimu kuhusu uwekezaji sambamba na kujadili mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka maazimio baina ya wawekezaji na Manispaa ya Temeke kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda aliyekuwa mgeni rasmi amesema Serikali inahitaji nguvu ya uwekezaji ili iweze kukusanya mapato na kutoa huduma bora Kwa wananchi.

"Serikali ili ifanye kazi vizuri inahitaji ushiriki wa karibu sana wa sekta binafsi, ndio maana leo Manispaa ya Temeke imeona ni busara tukutane hapa tujadiliane changamoto zinazotukabili, tupeane fursa zilizoko na ninyi wawekezaji mtusaidie kutupa maneno ya busara na hekima namna bora ya kufanya mazuri zaidi" alisema Mhe. Mapunda

Mapunda ametoa mwito kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo Temeke za kiuwekezaji na kuwahakikishia ushirikiano pamoja na mazingira bora yanayofaa kwa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

"Ujio wa bandari mpya utabadilisha jiji la Dar es salaam, kwahiyo ni fursa wana Temeke tunayo,Wekezeni Temeke. Msiogope Serikali yenu ni Serikali sikivu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda na anawaalika karibuni sana kuwekeza katika nchi yetu" amesema Mapunda

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya amesema dhamira ya Serikali ni kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta zote.

Ametoa rai kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali hususani kwenye maeneo ya kimkakati kama vile uwekezaji katika hoteli za kisasa, viwanda, makazi, viwanja vya michezo, bandari kavu, kilimo na kadhalika

"Manispaa ya Temeke imesheheni fursa nyingi za kiuwekezaji na kiuchumi, tuna maeneo takribani 25 ambayo yanaweza kuchukuliwa kwa ajili ya uwekezaji kulingana na malengo ya Manispaa.

" Hivyo nitoe mwito kwa wawekezaji kuwekeza Temeke na sisi kama Manispaa tumejipanga vema na tupo tayari kushirikiana katika kuimarisha kipato cha wawekezaji, uchumi wa halmashauri na Nchi yetu kwa ujumla." Amesema.

Kongamano Hilo limefanyika katika ukumbi wa DYCC Chang'ombe likiambatana na uzinduzi wa dawati la uwekezaji kwa ajili ya kuratibu shughuli za uwekezaji. Limehudhuriwa na taasisi mbalimbali ikiwemo TIC, TRA, TCCIA, NSSF,TPDC, TPSF, DCB Bank na kadhalika.


Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Temeke pamoja na viongozi wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Temeke mkoani Dar es Salaam katika picha ya pamoja
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya akitoa maazimio ya kongamano yaliyofikiwa baina ya Wawekezaji na Manispaa ya Temeke.
Mkuu wa idara ya Biashara, viwanda na uwekezaji Manispaa ya Temeke Ramadhan Gurumukwa akieleza jambo na wawekezaji katika kongamano la fursa za uwekezaji Temeke
Mkuu wa wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda akitoa hotuba yake katika kongamano la fursa za uwekezaji
Wawekezaji binafsi wakisikiliza kwa makini mawasilisho ya taasisi za serikali juu ya mazingira ya uwekezaji nchini

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...