Na Muhidin Amri, Tunduru

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Mbati wilayani Tunduru,wameiomba serikali kupitia wizara ya afya kuongeza kasi ya mapambano ya ugonjwa wa ukoma ili kuwanusuru na ugonjwa huo unaopoteza nguvu kazi ya vijana wengi katika kijiji hicho.

Wamesema hayo kwa nyakati tofauti,kwenye maadhimisho ya siku ya ukoma Duniani ambayo Kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Mbati kata ya Mbati.

Said Makunganya alisema,ugonjwa wa ukoma umechangia sana kuongezeka kwa umaskini katika kijiji hicho,kwani baadhi ya wagonjwa wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na kukosa tiba sahihi, hivyo kushindwa kufanya kazi za kujiletea maendeleo.

Amewaomba wataalam kutoka kitengo cha kifua kikuu na ukoma,kutembelea maeneo ya vijijini mara kwa mara ili kuwapata watu walioambukizwa ugonjwa huo ambao wameshindwa kwenda Hospitalini.

Said Ali alisema,kuwatembelea na kuwafikia wagonjwa wa ukoma wanaoishi vijiji vya pembeni ni jambo muhimu kwa sababu kama wataachwa bila kupata tiba sahihi wataendelea kuambukiza watu wengine katika jamii.

Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mbati Dkt Benjamin Matata alisema,homa ya ukoma na kifua kikuu katika kijiji cha Mbati ipo,kwani hata baadhi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa wanakuwa na dalili zote za ugonjwa huo.


Dkt Benjamin,ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitahada inazofanya katika kuzuia na kutokomeza ukoma na kifua kikuu kwa kuwezesha kampeni za uibuaji wa wagonjwa na kupeleka dawa kwenye zahanati na vituo vya afya vilivyopo pembeni mwa nchi.


Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia wizara ya afya,kuwaangalia wataalam na watumishi wake wanaofanya kazi maeneo ya vijijini ili waweze kuwafikia na kuwaibua wagonjwa wengi wenye matatizo mbalimbali waliopo kwenye jamii.


Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,Hospitali ya wilaya Tunduru kwa kushirikiana na mdau shirika la GRLA imeamua kufanya maadhimisho katika kijiji cha Mbati kutokana na kata ya Mbati kuwa na watu wengi walioambukizwa ugonjwa huo.


Alisema,licha ya jitihada zinazofanywa mara kwa mara na Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma za kutokomeza ugonjwa huo kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji na uchunguzi,lakini tatizo la ukoma katika kata hiyo ni kubwa ikilinganisha na kata nyingine za wilaya ya Tunduru.


Alisema, Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma itaendelea kufanya kampeni ya uelimishaji,na uibuaji katika maeneo yote yaliyoathirika zaidi hasa kando kando ya mto Ruvuma na watakaobainika kupata maambukizi ya ukoma wataanzishiwa dawa.


Kwa mujibu wa Mkasange,baadhi ya wagonjwa wanashindwa kufika katika maeneo ya huduma ya afya kutokana na kuogopa gharama na wengine kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya ugonjwa wa ukoma.


Dkt Mkasange alisema,kwa kawaida ukoma unaanza kujitokeza mwilini baada ya miaka 5 na kuendelea na ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya hewa kama ugonjwa wa kifua kikuu.

Ametaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni mgonjwa kutosikia baridi wala joto mwilini,kutosikia maumivu,macho kutoona vizuri,kukosa hisia sehemu iliyoambukizwa,kuwa na mabaka yenye rangi ya shaba na kukatika viungo.

Alieleza kuwa,ukoma unasababisha mgonjwa kupata ulemavu wa kudumu,kupata upofu na kuongezeka kwa umaskini katika familia na jamii na watu walioko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo ni wanaoishi kwenye nyumba zenye mwanga na hewa hafifu na wanaokaa na wagonjwa wa ukoma.

Mkasange,ameitaka jamii kutowatenga wagonjwa wa ukoma,badala yake kuwapa ushirikiano kwa kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kupata tiba sahihi.
 

 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mbati kata ya Mbati wilayani Tunduru,wakifuatilia elimu ya ugonjwa wa ukoma kutoka kwa mratibu wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani).

 

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akitoa elimu ya magonjwa ya ngozi kwa wananchi wa kijiji cha Mbati wilaya hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani ambayo kiwilaya  yamefanyika katika kijiji cha Mbati.
 

Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akimfanyia uchunguzi wa maginjwa ya ngozi mkazi wa kijiji cha Mbati  kata ya Mbati ambaye hakufahamika jina lake,wakati wa maadhimisho ya siku ya ukoma Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika kijiji hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...