Na. Peter Haule, WF, Dodoma

Norway imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kukijengea uwezo Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu kujenga Uchumi wa nchi.


Hayo yameelezwa jijini Dodoma, na Mhe. Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Tone Tinnes, kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.


Dkt. Nchemba alisema kuwa kiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona kuona sekta binafsi inashiriki katika kujenga Uchumi wa nchi, kutengeneza ajira kwa wananchi wakiwemo vijana na wanawake na kutengeneza vyanzo vipya vya kodi.


Aidha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa, Norway imepiga hatua kubwa katika eneo la kodi na kuishauri nchi hiyo iangalie namna ya kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana ujuzi katika eneo hilo na masuala mengine ya kifedha


Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Tabianchi, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa eneo hilo ni muhimu kwa Tanzania, ambapo ameiomba Norway ambayo imepiga hatua katika eneo hilo, kushirikiana na Tanzania ili iweze kupata vigezo muhimu vya kupatiwa fedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko hayo.


Dkt. Nchemba ameishukuru Norway kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, nishati, elimu, kilimo na ustawi wa jamii.


Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Tone Tinnes, alisema kuwa Ushirikiano wa nchi hizo mbili umetimiza zaidi ya miaka 60, na katika kipindi hicho nchi yake imeshiriki katika maendeleo kwenye Sekta za miundombinu, nishati, kilimo, na pia imeshiriki katika uanzishwaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na imechangia kujenga mitambo ya umeme wa maji.


Alisema kuwa katika eneo la Kilimo, nchi yake inaadhimisha miaka 50 ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa kutoa ujuzi na pia imekuwa na mchango wa ujuzi katika taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Fedha.


Mhe. Tone Tinnes, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kutoa kutoa ushirikiano katika kufanikisha mahitaji mapya ili kuharakisha maendeleo zaidi.


Alilitaja eneo mahususi ambalo nchi yake itashirikiana na Tanzania ni kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi jambo ambalo limekuwa na changamoto si tu kwa Tanzania nali pia Dunia nzima kwa ujumla, na kusisitiza kuwa kilimo kinatakiwa kutekelezwa kwa kuangalia athari ya mabadiliko ya Tabia nchi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akisalimiana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes, walipokutana ofisini kwakwe jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza katika kikao chake na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes, kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo, jijini Dodoma.


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (watatu kulia) akimsikiliza kwa makini Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes (wapili kushoto), walipokutana na kufanya mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma, kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.


Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes, akifafanua jambo katika kikao chake na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes (wa nne kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania pamoja na ujumbe wa Tanzania (Wizara ya Fedha), baada ya kumalizika kwa Kikao chao, jijini Dodoma, ambapo katika kikao hicho walijadili kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...