Wakazi saba wa Jijini Dar es Salaam, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni Dar Es Salaam walipofikishwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manne yakiwamo ya kusafirisha sukari na mafuta ya kupikia kwa magendo Vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 10.7.Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAKAZI saba wa Jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mbele ya mahakimu watatu tofauti wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manne yakiwamo ya kusafirisha sukari na mafuta ya kupikia kwa magendo Vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 10.7.

Mashtaka mengine ni kukwepa ushuru chini ya kifungu 148(e) cha sheria ya forodha, kusafirisha mizigo ya magendo kushindwa kuwasilisha nyaraka za bidhaa za magendo na kukutwa na bidhaa za magendo


Washitakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Veneranda Kaseko, Mahakimu Wakazi, Nabwike Mbaba na Ramadhani Rugemalira.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Anderson Lukosi akisaidiana na wakili kutoka TRA, Auni Chilamula amewataja washtakiwa hao kuwa ni Mfanyabiashara Mustapha Bakari (30) Mkazi wa Kunduchi, mafundi Mohamed Nassor(25) na Abdulmajid Kheri (17) na dereva Erick Solomon Mwagemba (25).

Wengine ni dereva Justin Mollel (35) pamoja na Wavuvi Mbaraka Mwanjovu (23) na Hamad Hamad maarufu Katoto (23).

Mbele ya Hakimu Nabwike Mbaba, washtakiwa Nassoro na Kheri wanadaiwa Februari 11, mwaka huu maeneo ya Kunduchi wilayani Kinondoni Dar es Salaam, walikutwa wakiingiza mifuko 20 ya sukari kwa kutumia njia ya magendo bila ya kulipa kodi na kukwepa ushuru wa Sh. 2,335,697.93 kinyume na sheria.

Inadaiwa siku hiyo pia washtakiwa hao walikwepa ushuru kwa kuingiza mifuko 20 ya sukari kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 956 BBF.

Pia huku pia wakishindwa kuwasilisha nyaraka za bidhaa za magendo pamoja na kukutwa na bidhaa za magendo.

Mbele ya Hakimu Kaseko, Erick anadaiwa kusafirisha mifuko 20 ya sukari kupitia bandari bubu na kukwepa ushuru wa Sh 2,335,697.93.

Mbele ya Hakimu Rugemalira, washitakiwa Mollel, Mwanjovu na Hamad, wanadaiwa kuwa, Februari 11 mwaka huu maeneo ya Mtongani - Kunduchi walisafirisha madumu 100 ya mafuta ya kupikia kupitia bandari bubu na kusababisha ukwepaji wa ushuru wa Sh 4,022,113.

Kwa upande wa Bakari anadaiwa kuwa Februari 11,2024 maeneo ya Mtongani Kunduchi, wilayani Kinondoni Dar es Salaam, kinyume na sheria aliingiza madumu 50 ya mafuta ya kupikia kupitia bandari bubu na kusababisha ukwepaji wa ushuru wa zaidi ya Sh milioni mbili.

Aidha inadaiwa Bakari akiwa dereva wa gari lenye namba za usajili T 964 DPJ aina ya Toyota Bravis alisafirisha madumu 50 ya mafuta ya kupikia yaliyotoka nje ya Tanzania

Pia inadaiwa katika tarehe na mahali hapo, Bakari alishindwa kuandaa taarifa ya usafirishaji wa madumu 50 ya mafuta ya kupikia huku akijua kuwa bidhaa hizo hazijalipiwa ushuru na kusababisha kukwepa kodi ya Sh 2,011,057.

Katika mashtaka ya nne, inadaiwa Bakari akiwa msimamizi na dereva wa gari lenye namba za usajili T 964 DPJ aina ya Toyota Bravis, kinyume na sheria alikutwa akisafirisha madumu 50 za mafuta ya kula yaliyokuwa yakitoka nje ya Tanzania huku akifahamu kuwa ni bidhaa ni za magendo.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi dhidi ya kesi hizo bado haujakamilika na kesi itatajwa tena Machi 21 mwaka huu. Washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...