NA VICTOR MASANGU KIBAHA

Jumuiya ya Umoja wa vijana ya Chama cha mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kibaha mji umempongeza kwa dhati mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji Selina Koka kwa kuona umuhimu wa kuwasapoti vijana kwa kutoa msaada wa mahitaji na vitu mbali mbali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa kwa vijana.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kibaha mjini Gamalu Makona wakati wa halfa fupi ya kukabidhiwa baadhi ya mahitaji na vitu mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa hamasa ambao wapo katika mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na kuupokea Mwenge wa uhuru.

Aidha Katibu huyo alisema kwamba Mama Koka amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia mambo mbali mbali katika jumuiya ya vijana katika Jimbo la Kibaha mji.

Aliongeza kwamba Mama Koka amewashika mkono na kuwapatia msaada wa vyakula mbali mbali,sambamba na mabati viti meza kwa ajili ya ujenzi wa banda ambalo litakuwa linatumika kukutana vijana wa uvccm pamoja na kupumzikia ili kujadili mambo ya jumuiya na maendeleo.

"Kwa kweli tunamshukuru na kumpongeza Mama Koka kwa kuwa na upendo wa kipekee maana hivi karibuni alikuja kututembelea umoja wetu na kile ambacho alituahidi kiukweli amekitekeleza na Mungu aweze kumbariki yeye pamoja na Mbunge kwa kuwa na moyo wa kujitolea,"alisema Katibu.

Akikabidhi msaada huo wa vitu mbali mbali kwa niaba ya Mama Koka Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Method Mselewa alisema kwamba msaada huo ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya mke wa Mbunge kwa vijana hao ambayo aliitoa alipokwenda kuwatembelea hivi karibu.

Katibu Method alisema Mama Koka anatambua mchango mkubwa ambao unafanywa na jumuiya ya vijana hivyo akaamua kutoa mahitaji mbali mbali ambayo yatawasaidia vijana pindi wanapokuwa wakiendelea na mazoezi yao ya kujiandaa na Mwenge wa uhuru.

Mselewa alibainisha kwamba vijana hao ni Taifa la kesho hivyo wanapaswa kupendana na kuwa na maadili mazuri pamoja na uzalendo kwani ndio viongozi watarajiwa katika siku za usoni.

"Hapa nimekuja kwa niaba na mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Koka na nimekuja na vitu mbambali kwa ajili ya chakula pamoja na redio ambayo mtakuwa mkiitumia katika burudani na mambo mengine,"alifafanua Katibu huyo.

Aliwahimiza vijana kuendelea kufanya mazoezi pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuupokea Mwenge wa uhuru ambao utatembelea miradi mbali mbali ya maendeleo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimon ambaye naye alifika kuwajulia hali vijana hao wa hamasa amewahimza kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika ujio wa mapokezi ya mbio za Mwenge wa uhuru na kwamba serikali ipo pamoja nao.

Katika hatua nyingine aliwaahidi katika mkesha wa mwenge kutakuwa na burudani mbali mbali za wasanii wakubwa pamoja na wasani wa kibaha na kwamba siku hiyo wategemee kuona burudani ya aina yake hivyo wajitokeze kwa wingi.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...