WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa rai kwa wadau wa maendeleo nchini likiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kuiunga mkono Serikali katika uelekeo wake wa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kuondoa umaskini kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara ambapo walijadili kuhusu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Serikali na Shirika hilo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa taasisi za Kiserikali na zisizo za kiserikali ziunganishe nguvu ili kuwawezesha wananchi katika maeneo ya uzalishaji na sio semina kwa kuwa kuwekeza kwenye semina hakumuondoi mwananchi kwenye umasikini.
“Tuliishafanya sana semina, kuongeza uwezo, huu si muda tena wa mbia anasema anakuja kusaidia halafu anasaidia kwenye semina, tuliisha jifunza vya kutosha, tujielekeze kwenye shughuli za uzalishaji, aje mdau aseme Serikali imejenga Skimu kubwa ya umwagiliaji, mimi najenga hii ya mbogamboga kwa ajili ya wanawake wazalishe mwaka mzima”, alisema Dkt. Nchemba.
Alitoa rai kwa Shirika la UNDP kusaidia kupeleka ujumbe huo kwa wadau wengine, katika kipindi ambacho Serikali imeweka uelekeo kwenye sekta za uzalishaji basi na wadau wengine wote wa maendeleo nchini wachukue mwelekeo huo ili kuweza kuunganisha nguvu katika maeneo hayo ya uzalishaji.
Aidha alisema kuwa katika mazungumzo yao wamejadili maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kitaalamu katika maeneo ya kuongeza uwekezaji ambayo yanaenda sambamba na ajenda kuu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza uwekezaji unaolenga kuongeza ajira kwa watanzania hasa vijana, ushirikiano katika Dira Mpya ya Maendeleo inayoandaliwa na dhana pana ya Uchumi jumuishi usiomuacha mtu yeyote nyuma.
Vilevile alisema kuwa imani yake ni kuona ushirikiano wa kimaendeleo utaendelea chini ya Awamu mpya ya Mfumo wa Ushirikiano Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) wa mwaka 2022 hadi 2027, ambao unahusisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Mashirika yaliyo chini yake na Serikali ya Tanzania.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara alisema kuwa anafurahishwa na Tanzania kwa kuwa inasonga mbele kutoka uchumi wa chini na kuwa uchumi wa kati.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zinampa ujasiri kusema ni rahisi uchumi wake kukua kwa kuwa unajengwa kwenye amani, umoja na mshikamano, ambapo jumuiya za kimataifa zinathamini hali hiyo na pia zinamatarajio makubwa kuwa Tanzania itaendelea kuzalisha taarifa nzuri kwa Afrika na Dunia kwa ujumla na kujenga Uchumi jumuishi.
Aidha, alisema kuwa uwekezaji kwa ajili ya baadae utaiwezesha Tanzania kusonga mbele na pia amekaribisha majadiliano kati ya Serikali na Shirika hilo yatakayowezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo kwenye sekta za uzalishaji.
Bw. Komatsubara ameishukuru Tanzania kwa kumpa nafasi kufanya kazi kwa Watanzania na Serikali yake na ameahidi kuongeza ushirikiano kati ya Shirika lake na Serikali na pia kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika Shirika hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...