Na Mwandishi wetu, Mirerani

MAMIA ya wakazi wa Jiji la Dar es salaam, jiji la Arusha na wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamejitokeza kwa wingi kumzika mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Abraham Sumari (Simango).

Marehemu Sumari ambaye ni baba mzazi wa msanii Nakaaya na Miss Tanzania mwaka 2005 na Miss World Africa 2005, Nancy amezikwa jana jumatano Mei 15 mwaka 2024.

Nancy Sumari akizungumza kwenye maziko hayo amemshukuru Mungu kwa maisha mema aliyoishi baba yao hapa duniani na kuona safari yake ya mwisho kwenye nyumba yake ya milele.

Nancy amesema wamefarikija kwa watu wengi kujitokeza kwenye safari ya mwisho ya marehemu baba yao na kueleza mafanikio mengi ya jamii yaliyofanyika kupitia yeye.

Amesema baba yao amewafundisha kutokata tamaa na kutoogopa kwani hata akiwa mgonjwa hospitalini hakuwa analalamikia maumivu ila aliwapa faraja na kuwatoa hofu.

"Alikuwa ni baba mpambanaji na hata akiwa kwenye kuvuta pumzi yake ya mwisho tulikuwa kwenye sala na kuimba nyimbo za sifa za kuabudu," amesema Nancy.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Justin Nyari amesema wayaendeleza mema yote aliyowaasa wakati wa uhai wake.

Nyari amesema marehemu Sumari alikuwa mpenda maendeleo aliyewaasa vijana kila wakati wasikate tamaa katika kutafuta maisha.

"Marehemu alikuwa mpenda maendeleo ambaye aliwaunga mkono vijana wapambanaji katika utafutaji hasa alipokuwa Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini kipindi hicho tukiwa mkoa wa Arusha (AREMA)," amesema Nyari.

Diwani wa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani, Lucas Zacharia amesema marehemu mzee Sumari ameacha alama ya maendeleo kwenye eneo hilo.

Zacharia amesema mzee Sumari alijitolea eneo la zaidi ya ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa taasisi mbalimbali za serikali zinazotumika hadi sasa.

"Sisi tuliobaki hai tunapaswa kujiuliza je tunaiachia nini Mirerani wakati tukiwa hai kwani marehemu mzee Sumari tumeona alama alizoziacha nanzisizofutika kwa kizazi hadi kizazi," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula amesema marehemu mzee Sumari atakumbukwa kwa maendeleo yaliyofanyika kupitia mashamba aliyokuwa akiyamiliki.

Chengula ametaja baadhi ya taasisi zilizojengwa kwenye mashamba yake ni kituo cha polisi Mirerani, kituo cha afya Mirerani, shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa na zilipo ofisi za mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani.

Marehemu mzee Sumari ambaye alizaliwa Oktoba 10 mwaka 1952 mkoani Arusha, alifariki dunia jijini Dar es salaam Mei 13 mwaka 2024.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...