Na MWANDISHI WETU.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya kuelezwa mafanikio mbalimbali ambayo NSSF imeyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 13 Julai, 2024 wakati alipotembelea banda la NSSF kwenye kilele cha Wiki ya Wazazi iliyofanyika Mjini Mpanda Mkoani Katavi. NSSF imeshiriki katika kutoa elimu ya hifadhi ya jamii katika maadhimisho hayo kwani Jumuiya ya Wazazi ni mojawapo ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele amesema NSSF inamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa namna alivyofungua nchi, ambapo wafanyakazi kwenye sekta binafsi wakiwemo wale wa viwandani wameongezeka na kuiwezesha NSSF kupata wanachama wapya.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya, umefungua fursa mbalimbali ambapo wakati unaingia madarakani mwaka 2021 thamani ya NSSF ilikuwa ni Shilingi Trilioni 4.8 lakini sasa imepanda kwa juhudi kubwa ambazo umefanya tumefikia Trilioni 8.5,” amesema Bi. Mengele.

Amesema NSSF inaendelea kuboresha mifumo yake ya TEHAMA ambapo hivi sasa mwajiri anaweza kumwandikisha na kuwachangia wafanyakazi wake kulekule walipo na pia mwanachama anaweza kuangalia taarifa zake mbalimbali bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF na kwa hatua hiyo imerahisisha huduma kwa wanachama.

Akizungumzia ushiriki wa NSSF katika Kilele cha Wiki ya Wazazi, Bi. Lulu alimueleza Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa NSSF imeshiriki Maonesho yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi kwa kuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Wazazi ni wanachama wa NSSF kama zilivyo Jumuiya nyingine za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Bi. Lulu amesema wametumia maonesho hayo kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama waliotembelea kwenye Banda hilo, matumizi ya mifumo kwa waajiriwa na waajiri ambapo wakiwa popote wanaweza wakapata taarifa zao za michango na kuwasilisha michango bila kulazimika kutembelea ofisi za NSSF.

Amesema NSSF inaendelea kufanya vizuri kwa kuweka kipaumbele cha kuwarahishia huduma wanachama wake.
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...