Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Utafiti uliofanywa jijini Dar es salaam na maeneo mengine ya dunia umeonesha kuwa kuwahusisha wanafunzi kwenye shughuli mbalimbali na matukio ya kisayansi kunasaidia kuongeza uwezo wao wa udadisi na  kupenda masomo ya sayansi.

Profesa mbobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Ndaki ya Sayansi asili na Tumizi Prof. Faith Mabiki akaizungumza na wanafunzi wa mchepuo wa sayansi kwenye shule ya ALFAGEMS ya Mkoani Morogoro.

Kauli hiyo imetolewa na Profesa mbobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Ndaki ya Sayansi asili na Tumizi Prof. Faith Mabiki wakati akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya ALFAGEMS iliyopo Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro katika mafunzo maalumu iliyoandaliwa na wananchama wa Pan African Chemistry Network kwa lengo la kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi hususani kemia.

“Tupo hapa leo kwakuwa tunaamini katika utafiti huo kwamba tunahitaji kuwashirikisha watoto wetu kwenye matukio ya kisayansi ili kukuza udadisi wao na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ambayo watu huamini kuwa ni magumu lakini kupitia mafunzo ya aina hii kwa vitendo mara kwa mara na kuipenda kemia wanaweza kuona kuwa masomo ya sayansi sio magumu kama inavyodhaniwa” Alieleza Prof. Mabiki.

Prof. huyo wa Kemia kutoka Ndaki ya Sayansi Asili na Tumizi (CoNAS) SUA amewataka kutambua kuwa nchi inahitaji wakemia wengi ili kusaidia kufanya kazi kwenye viwanda mbalimbali ambavyo Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kujenga kwakuwa bila kufanya hivyo nafasi hizo zitachukuliwa na wageni.

Amewataka wanafunzi hao na wengine nchini kuona nafasi ya kemia kwenye maisha ya kila siku kwenye kila eneo la maisha akitolea mfano wingi wa bidhaa zinazoongoza kwa kutumiwa madukani zinazotengenezwa kupitia uchanganyaji wa kemikali mbalimbali na kupata bidhaa pendwa kwa jamii ikiwemo vinywaji, hivyo mafunzo ya iana hiyo yatasaidia kuzalisha idadi ya wanakemia wengi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Mkemia Dkt. Frank Rwegoshora amesema kuwa mafunzo ya aina hiyo ni muhimu sana kwa wanafunzi hao ambao wana mapenzi na masomo ya kemia na ukizingatiwa kuwa ndio wanatarajia kwenda kusoma vyuo vikuu wanahitaji kujua umuhimu na faida za kusoma kemia na fursa zilizopo duniani kupitia fani hiyo muhimu.

Mratibu wa mafunzo hayo Mkemia Dkt. Frank Rwegoshora akizungumza malengo ya mafunzo hayo.

“ Kwakweli tumefurahi sana sisi kama waandaaji lakini pia walimu na zaidi wanafunzi 150 ambao wamejitokeza kwa wingi na kufurahia mafunzo hayo yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yaliyotolewa na walimu na wabobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine na tunaamini tumezalisha jeshi la wataalamu wa kemia kupitia mafunzo haya” alieleza Dkt. Rwegoshora.

Dkt. Rwegoshora amesema wamefanikiwa kufikia wanafunzi wa shule hiyo leo lakini zipo shule nyingi nchini ambazo zina wanafunzi wa aina hiyo na wengine wenye uwezo mkubwa na mapenzi na kusoma kemia na kuwa wakemia, lakini wana woga na maneno ya baadhi ya watu kuwa kemia ngumu hivyo wanahitaji kufikiwa na kupewa moyo na kuoneshwa fursa zilizopo ikilinganishwa na masomo mengine.

“Tunatoa shukrani nyingi kwa wafadhili wa mafunzo haya Pan African Chemistry Network na Royal Society of Chemistry kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha hamasa hii muhimu kwa wanafunzi wetu na wanasayansi wachanga ambao wameonesha kufurahi na kuahidi kuchagua masomo ya kemia kwenye masomo yao ya ngazi za juu” alieleza Dkt. Rwegoshora.

Wakieleza furaha yao mara baada ya mafunzo hayo baadhi ya wanafunzi hao akiwemo Maganja Jeremiah amesema wamefurahi kutembelewa na wataalamu hao lakini kubwa zaidi mafunzo hayo yamewaonesha fursa kubwa zilizopo kwenye fani ya kemia pamoja na mchango wa wataalamu wa kemia kwenye maendeleo ya Viwanda na uchumi wa Taifa.

“Tunawashukuru sana hakika binafsi ninasoma mchepuo wa sayansi lakini nilikuwa na woga kuhusu swala la maisha baada ya kuhitimu chuo kikuu fani ya kemia, lakini kwa maelezo na ushahidi uliotolewa na wataalamu hawa kutoka SUA, sina woga tena na nitachagua kusoma SUA fani hii ili niisaidie nchi yangu” alisema Maganja.

Nae mwanafunzi Prosper Rey amesema kupitia mafunzo kwa vitendo wamejifunza vitu vingi ambavyo walikuwa hawavifahamu na kuahidi kuendelea kuvitumia kwenye maisha yao na kila siku nyumbani lakini pia kwenye masomo yao hasa wakati wa mitihani yao ya mwisho.

“Elimu hii itatuwezesha na sisi kuwa mabalozi wazuri wa masomo ya kemia kwa wanafunzi wenzetu na kwa jamii kuondoa woga uliosambaa miongoni mwa watu kuhusu ugumu wa masomo ya sayansi hasa kemia ili jamii zaidi ielewe na kuhamasika kuisoma na kuitumia kwenye maisha yao” Aalieleza Prosper.

Mafunzo hayo yametolewa walimu wa Kemia na Fizikia kutoka chuo hicho Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa ufadhili wa Pan African Chemistry Network na Royal Society of Chemistry.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAFUNZO HAYO

















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...