Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ruvuma limewataka wananchi kuacha woga wa kuwasiliana nao wakati wa majanga mbalimbali kama moto au uokoaji wa watu waliokwama, kwa kudhani kuwa kuna gharama zinazotozwa baada ya huduma hizo, hivyo wananchi wametakiwa kupiga namba ya dharura 114 bila kusita, kwani huduma zote za uokoaji hutolewa bila malipo yoyote.

Wito huo umetolewa leo na Mkaguzi wa Zimamoto Mkoa wa Ruvuma, Afande Jackson Mahali, kwa niaba ya Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, wakati wa ziara ya maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Good Shephard, kilichopo mjini Songea.

Afande Mahali amesema kuwa hata kama waokoaji watakaa kwenye eneo la tukio kwa zaidi ya siku mbili, wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu gharama, kwani huduma hiyo ni sehemu ya majukumu ya serikali katika kulinda maisha na mali za wananchi.

Katika maadhimisho hayo, Jeshi la Zimamoto linatoa elimu ya uzimaji moto na namna ya kutoa taarifa za majanga, kwa lengo la kuwajengea jamii, hasa watoto, uelewa wa jinsi ya kuwasiliana na Jeshi hilo pindi majanga yanapotokea. Amewaasa wanafunzi na jamii kwa ujumla kuendelea kutumia namba 114 kwa dharura yoyote inayohitaji msaada wa haraka kutoka kwa Jeshi hilo.

Mbali na kutoa elimu, Jeshi la Zimamoto pia limekabidhi mahitaji mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za malezi na kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji muhimu ya maisha.

Kwa upande wake, mlezi wa kituo hicho, Bi Agnetha Nchimbi, ameushukuru uongozi wa Jeshi la Zimamoto kwa ujio wao na msaada walioutoa. Amesema kitendo hicho ni ishara ya upendo na mshikamano na ametoa wito kwa Jeshi hilo kuendelea kuwatembelea mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya watoto hao.

Wiki ya Zimamoto itaendelea hadi Jumapili, Mei 4, 2025, ambapo kilele chake kitaadhimishwa kwa utoaji wa elimu katika stendi ya Mfaranyaki mjini Songea. Aidha, kesho Mei 3, kutakuwa na bonanza maalumu ikiwa ni sehemu ya kuelekea tamati ya maadhimisho hayo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...