



Na Fredy Mgunda, Kilwa Lindi
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa, Mheshimiwa Kuruthum Issa Runje, imefanya ziara maalum Wilayani Kilwa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.
Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya Shilingi 44,551,077,124.12. Miradi hiyo inahusisha nyanja mbalimbali muhimu kwa ustawi wa wananchi wa Kilwa, ikiwemo maji, elimu na afya.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na Mradi wa Maji kwa Miji 28 ambao unagharimu Shilingi 44,007,870,224.12. Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilwa.
Pia kamati ilikagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Sekondari ya Mavuji (Shilingi 95,000,000), ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Msingi Naipuli (Shilingi 64,000,000), na ujenzi wa jengo la Vijana Rika katika Kituo cha Afya Tingi (Shilingi 22,006,900). Aidha, walitembelea mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa manne na vyoo katika Shule ya Sekondari Mtanga wenye jumla ya thamani ya Shilingi 362,200,000.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhe. Kuruthum Issa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Baraza la Madiwani na watendaji wote kwa usimamizi thabiti na utekelezaji bora wa miradi hiyo. Alieleza kuwa utekelezaji huo unaonesha namna ambavyo Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
“Tunafurahishwa na kasi na uwajibikaji wa viongozi wetu wa Wilaya ya Kilwa katika kutekeleza Ilani ya Chama. Ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa Serikali, CCM na wadau mbalimbali ni mfano wa kuigwa. Tuendelee kuchapa kazi kwa kushirikiana ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mhe. Kuruthum.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa chama hicho kuhakikisha kuwa ahadi zake kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi zinatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo kwa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...