Katika sekta ya usafiri wa mtandaoni inayokua kwa kasi nchini Tanzania, si jambo geni kwa wateja waliobobea kidijitali kukumbana na madereva wasio waaminifu.


Dora Godson, mkazi wa Njiro anayesafiri kila asubuhi kwenda kazini Burka kwa kutumia app ya usafiri, anakumbuka tukio ambapo dereva mmoja alianza safari bila kumpakia na kuhitimisha safari hiyo, na hivyo kutoza kadi yake ya Mastercard moja kwa moja.

Ingawa alirejeshewa fedha baada ya kuripoti kupitia app, anasema tukio hilo hua linaongezaga ucheleweshaji wa safari. Kampuni inayoongoza katika usafiri wa mtandaoni nchini, Bolt Tanzania, imeitikia changamoto kama hizi kwa kuzindua huduma mpya ya “Pick-up Code” inayolenga kuimarisha usalama wa abiria na uhalali wa miamala ya kidijitali. Kupitia huduma hii, app ya Bolt hutengeneza nambari ya siri ya usafiri (Pick-up Code) kila mara abiria anapoweka oda.

Safari inaweza kuanza tu baada ya abiria kumtajia dereva nambari hiyo, hatua ambayo huongeza ulinzi kwa pande zote mbili. “Ubunifu huu unakabiliana moja kwa moja na matatizo yanayojirudia mara kwa mara kwenye sekta ya usafiri wa mtandaoni,” alisema Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania na Kenya.

“Kwanza, madereva wanaoanza safari bila kumpakia abiria anayelipa kwa kadi. Pili, utambuzi usio sahihi wa madereva — jambo linaloweka abiria kwenye hatari ya kupakia madereva feki au hatari.” Kwa kuunganisha kuanza kwa safari na uthibitisho wa abiria, Bolt inalenga kuhakikisha madereva halali pekee ndio wanaoendesha safari, na hivyo kupunguza safari hewa zinazolipwa bila huduma kutolewa. “Pick-up Code inawapa abiria uwezo zaidi, inalinda malipo, na inadhihirisha dhamira yetu ya kulinda usalama wa kidijitali katika usafiri,” aliongeza Dimmy.

Wateja wanaotumia njia ya malipo ya kielektroniki wanakumbushwa pia kuhakikisha madereva wanabofya ‘end trip’ mara baada ya kufika walipoelekezwa. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hadi mwaka 2022 kulikuwa na zaidi ya pikipiki za usafirishaji 600,000 zilizokuwa zimesajiliwa nchini.

Idadi rasmi ya teksi za magari bado haijatangazwa, lakini inaaminika kuwa idadi hiyo inaongezeka kadri vijana wengi wanavyoingia kwenye sekta ya usafiri wa mtandaoni kama suluhisho la ukosefu wa ajira. Kadri idadi ya madereva na abiria inavyozidi kuongezeka, matarajio ya ubunifu zaidi na hatua za kiusalama pia yanapaswa kuimarishwa ili kulinda usalama wa pande zote katika mfumo wa usafiri wa kisasa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...