Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha 21 Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei, 2025.
Ofisi ya Makamu wa Rais imesema mchakato wa kulipa mamlaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kupitia mchakato unaoendelea.
Kuifanya NEMC kuwa mamlaka kutaipa nguvu ya kisheria ya kusimamia majukumu yake ipasavyo na hivyo kujiwezesha kimapato.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei, 2025 wakati akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Mpendae Mhe. Toufiq Salim Turky lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti maalumu Mhe. Amina Ali Mzee aliyetaka kujua ni lini mchakato wa NEMC kuwa mamlaka kamili.
Mhe. Khamis amesema Mchakato wa kulifanya Baraza hilo kuwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) tayari umekwishaanza na pindi utakapokamilika utawasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa maamuzi.
Alifafanua kuwa changamoto inayosababisha kuchelewa kwa vyeti vya tathmini ya athari kwa mazingira ni mifumo kuwa na changamoto hivyo kutumia muda mrefu wa kuviandaa.
Halikadhalika Naibu Waziri Khamis alisema kuwa baadhi ya miradi inachelewa kwasababu ya kukosa vigezo ambavyo vinataka maeneo ambako miradi inatekelezwa kulinda mazingira na afya.
“Niwapongeze mamemja wa kanda wa NEMC wakimsaidia mkurugenzi wanafanya kazi nzuri mnajitahidi kuhakikisha zoezi la utoaji wa vyeti linafanyika kwa haraka pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zikiwemo ucheleweshaji wa tarifa kutoka kwa wataalamu za waelekezi,” alisema.
Awali katika swali lake la msingi, Mhe. Turky alitaka kujua kuna mpango gani wa kutatua changamoto za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) hususan za kibajeti ili iweze kushughulikia athari zitokanazo na uchafuzi wa mazingira nchini.
Akijibu swali hilo, Mhe. Khamis alifafanua kuwa NEMC imekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoathiri utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hizi hususani za kibajeti, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo Kufanya mapitio ya Kanuni za Ada na Tozo za mwaka 2021 na kuongeza vyanzo vipya vya mapato na viwango vya tozo kwa miradi mikubwa ambayo shughuli zake zina athari kubwa kwenye mazingira.
Alisema Serrikali inaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa matumizi ya kanuni mpya ya Ada na Tozo ya mwaka 2024, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ambayo inarahisisha ukusanyaji wa ada kwa ajili ya undeshaji wa shughuli za Baraza na kuboresha Kanzidata ya miradi yote inayotakia kulipa ada na tozo za Mazingira.
Naibu Waziri Khamis ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya kaguzi za kimazingira katika miradi mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu na kuhimiza ulipaji wa ada na tozo za mazingira.
Pia, kuongeza idadi ya watumishi na kuanzisha Ofisi za Kanda ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi na kuwafikia wadau wengi kwa muda mupi katika maeneo mbalimbali nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...