Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MRADI wa Kilimo na Lishe NOURISH Tanzania, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo Norway (Norad) na kutekelezwa na wadau wa maendeleo SNV pamoja na Farm Africa kupitia washirika wake RECODA na MIICO wameandaa siku ya wakulima wa mradi huo katika wilaya 10 ndani ya mikoa mitano ya Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida, na Songwe.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Kijiji cha Nghumbi, Halmashauri ya Kongwa, mwishoni mwa wiki, Ofisa wa Mradi wa NOURISH, Theophil Tarm, amesema wamelenga kutoa elimu kwa wakulima wanufaika wa mradi pamoja na jamii nzima ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na elimu ya lishe, usafi wa mwili na mazingira pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ambayo itawasaidia kuongeza kipato.

Amesema kuwa sambamba na hayo pia watapata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya mfano yaliyofanikiwa, kuunganishwa na biashara za kilimo na kuongeza maarifa kupitia mapishi vinavyoonyesha lishe bora pamoja na burudani za kitamaduni.

“Mradi wa NOURISH wilayani Kongwa umefanikiwa kuelimisha juu ya utengenezaji wa bustani za nyumbani 177, kuwaunganisha wakulima na kampuni za pembejeo bora za kilimo (mbegu, viatilifu na machine), kuanzisha vikundi vya kilimo 47 vikiwa na jumla ya wanachama 1,880 pamoja na mashamba darasa 47 na kusambaza miche takribani 28,000 ya viazi lishe,” amesema.

Aidha, Tarm ameongeza kuwa, pia mradi wa NOURISH umefanikiwa kuwapa wakulima pembejeo za kilimo kwenye mashamba darasa ambapo wametoa jumla ya kilogram 825 za mbolea za kupandia na kilogram 525 kukuzia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa siku ya wakulima wa NOURISH katika Halmashauri ya Kongwa ametoa wito kwa wakulima washiriki wa mradi kuwa na chachu ya maendeleo kwa kuyatekeleza kwa vitendo kwenye kaya zao yale waliyofundishwa lakini pia kushirikiana katika vikundi na wataalamu wa kilimo na wakulima viongozi.

“Nashauri serikali za vijiji zihakikishe mmesimamia sheria ndogo ndogo (by-laws) bila upendeleo ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya vikundi na teknolojia zilizoletwa hata baada ya mradi huu kufikia tamati,” amesema Mayeka.

Aidha amewataka wanaofanyakazi kwenye vikundi kupanua wigo kwa kuwa na umoja na ushirikiano katika kutekeleza mradi huo.

“Mnaofanya kazi kwenye vikundi hakikisheni mnapanua wigo na ushirika mpana zaidi; hakikisheni vikundi vinasajiliwa na kuwa na ushirika wa mazao mbalimbali.” ameongeza Mayeka.

Hadi sasa, katika mikoa mitano yaani Dodoma, Manyara, Singida, Songwe na Rukwa, Mradi wa NOURISH Tanzania umeimarisha kwa kiasi kikubwa mifumo ya kilimo ndani ya mwaka mmoja ambapo wakulima zaidi ya 6,000 wameunganishwa na wasambazaji wa pembejeo.

Amesema watoa huduma 472 wa afya ya jamii wamefundishwa kuhusu lishe bora na zaidi ya wakulima viongozi 400 wamepata mafunzo ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.

“Hatua hizi ni mwanzo wa mabadiliko ya kudumu, yakilenga kuongeza uzalishaji,” amesisitiza

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...