Tunduru–Ruvuma
Mradi wa Maji Msuguri–Mchoteka unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kwa ufadhili wa Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF), umeanza kuleta mabadiliko makubwa ya kiafya na kimazingira kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, hasa katika vijiji saba vinavyonufaika moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru Mhandisi Maua Joseph Mgallah, mradi huo umefikia asilimia 85 ya utekelezaji na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 2. Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa tenki la maji la lita 500,000, nyumba ya mitambo, vituo 12 vya kuchotea maji, banio la kuelea, ufungaji wa mifumo ya nishati ya jua na pampu, pamoja na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 9,849.
Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuhudumia wananchi 16,124 kutoka vijiji vya Masuguru, Mchekeni, Mchoteka, Mkolola, Mnemasi, Likweso na Kitani. Kupitia upatikanaji huu wa maji safi, kiwango cha huduma hiyo katika Wilaya ya Tunduru kitaongezeka kutoka asilimia 81.86 hadi asilimia 86.65, hatua inayochochea uboreshaji wa afya ya jamii kwa kupunguza magonjwa yatokanayo na maji machafu.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mchoteka, Bi. Amina Omari, alisema:
“Tulikuwa tunatesekasana, maji yalikuwa mbali na si salama. Lakini sasa tuna matumaini mapya, tunaona maisha yakibadilika."
Wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi, amewataka wananchi kushirikiana na viongozi wa vijiji kuutunza mradi huo mara utakapoanza rasmi kufanya kazi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya maji kwa manufaa ya kila Mtanzania.
Mradi wa Msuguri–Mchoteka ulianza kutekelezwa tarehe 12 Februari 2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Julai 2025, chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi ya RJ Construction Company Limited-Time.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada madhubuti za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kuwa huduma muhimu kama maji safi zinawafikia Watanzania waishio vijijini, kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...