Tandahimba, Mtwara

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tandahimba umetenga Shilingi 452,500,000 kwa ajili ya kuchimba visima vitano vya maji safi na salama katika vijiji vya Mivanga, Lyenje, Dinduma, Mchangani na Michenjele, kwa lengo la kuondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba, Falaura Kikusa alisema kuwa mradi huo ni sehemu ya Programu Maalumu ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inayolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama.

“Mradi huu ni mkakati maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupunguza adha ya maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hii muhimu. Utekelezaji wake ulianza Mei 2024 na unatarajiwa kukamilika Juni 2025 kutokana na changamoto mbalimbali, licha ya mpango wa awali kumalizika Disemba 2024,” alisema Kikusa.

Kikusa alieleza kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 76, ambapo miundombinu ya maji ikiwemo usimikaji wa matanki ya lita 10,000 imekamilika katika vijiji viwili vya Mivanga na Lyenje, huku usimikaji wa pampu na mifumo ya nishati ya jua ukiwa umefanyika katika vijiji vya Mivanga, Lyenje, Dinduma na Mchangani.

Kwa mujibu wa Kikusa, gharama ya kisima kimoja ni Shilingi 90,500,000 na hadi sasa Shilingi 124,106,686.40 kati ya fedha zilizotengwa tayari zimelipwa. Fedha hizo zinatokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo mpango wa Lipa kwa Matokeo, Mfuko wa Taifa wa Maji na michango ya wadau wa maendeleo.

Aidha, alisema mradi huo umetoa ajira za muda mfupi kwa wananchi wa maeneo husika wakiwemo mafundi, wapishi, na madereva, huku pia ukichochea maendeleo ya kilimo na kusaidia kupunguza magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara.

Katika kijiji cha Mivanga, kisima kimoja kina uwezo wa kuzalisha maji lita 372,000 kwa siku. Wananchi wa vijiji hivyo wametoa maeneo ya ujenzi wa visima hivyo bila fidia, yenye thamani ya takriban Shilingi 2,500,000.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Katani Ahmed ameishukuru serikali kupitia RUWASA kwa kutekeleza mradi huo muhimu na kusisitiza kuwa umeleta afueni kubwa kwa wananchi waliokuwa wanatumia gharama kubwa na muda mwingi kutafuta maji.

Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujali ustawi wa wananchi wa Tandahimba na kuwataka wakazi wa vijiji walionufaika na mradi huo kushirikiana na serikali kuutunza ili udumu kwa muda mrefu.

Mkazi wa kijiji cha Mivanga, Bi. Asha Seleman alisema mradi huo umesaidia kupunguza gharama za maisha kwa wakazi wa kijiji hicho kwani hapo awali walikuwa wananunua ndoo moja ya maji ya lita 20 kwa Shilingi 1,000.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...