Na MWANDISHI WETU,
MWANZA. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hoteli ya nyota tano ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), inayojengwa katika eneo la Capripoint jijini Mwanza, itakayoendeshwa na kampuni ya kimataifa ya RADISSON.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mhe. Mtanda alisema ameangalia chumba cha mfano kilichojengwa na kampuni ya RADISSON ambacho kitakuwa mfano wa vyumba vyengine vyote 183 vinavyoendelea kujengwa kwa ubora wa hali ya juu.

“Nimefarijika kuona maendeleo ya ujenzi yakiendelea kwa ubora wa hali ya juu. Leo nimeona chumba cha mfano kati ya vyumba 183 vinavyotarajiwa kukamilika, vyote vikiwa na muonekano mmoja ambao unaangalia Ziwa Victoria. Kukamilika kwa hoteli hii kutaliwezesha jiji letu kuwa na miundombinu ya kisasa ya kupokea wageni wa kitaifa na kimataifa”, alisema Mhe. Mtanda.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza NSSF kwa uwekezaji wa mradi huo na kuwa ameona viwango vya mwendeshaji wa hoteli hiyo kuwa vinavutia ikiwemo chumba hicho cha mfano ambacho kinavutia.

Mhe. Mtanda aliishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mradi huo kuendelea na kuwa amekuwa akifuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo.

“Kwa hiyo nawapongezeni sana NSSF kwa uwekezaji huu mkubwa ambao ukikamilika utakuwa na tija kubwa kwa uchumi wa Kanda ya Ziwa, kuimarisha sekta ya utalii na kufungua fursa mpya za ajira kwa wananchi”, alisema Mhe. Mtanda.

Alisema kupitia mradi huo na mingine ya kimkakati kama vile uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwanza, meli ya Mv. Mwanza na reli ya SGR, jiji hilo litafikika kwa urahisi na kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji na utalii kwa upande wa Kanda ya Ziwa.

Alisema kwa sasa Mkoa wa Mwanza unachangia asilimia 7.2 katika pato la Taifa, lakini kutokana na miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa ukiwemo wa hoteli hiyo, mchango huo unaweza kufikia asilimia 10.

Akielezea umuhimu wa uwekezaji huo, Mhe. Mtanda alisema uwepo wa hoteli ya kiwango cha kimataifa ni hitaji la msingi kwa miji inayokua haraka kama Mwanza, hivyo utakapokamilika utachochea fursa za kiuchumi na kukuza utalii.

Naye, Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF, Bw. Gabriel Silayo, alisema mradi huo umefanyiwa utafiti wa kina na utaleta faida kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, nikuhakikishie kuwa tumefanya utafiti na tumeona kuwa mradi huu utalipa. Kama ulivyojionea tumempata wendeshaji wa kimataifa RADISSON ambaye ana hoteli zaidi ya 12,000 duniani kote, zikiwemo zaidi ya 98 barani Afrika”, alisema Bw. Silayo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo kutoka Afrika Kusini, Bw. Gehan Nel alisema atahakikisha anasimamia mradi vizuri ili kukidhi ubora wa hoteli zingine za RADISSON duniani na amepongeza serikali ya Tanzani kwa kuruhusu wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

Alisema kwa kushirikiana na NSSF atasimamia mradi huo ili ukamilike kwa haraka kwani hoteli hiyo imejengwa katika mandhari ya kuvutia kando ya Ziwa Victoria na itachochea wageni wengi kufika nchini.

Uwekezaji huu ni moja kati ya majukumu ya Mfuko wa NSSF kuwekeza sehemu mbalimbali ili kuhakikisha inalinda thamani ya michango ya wanachama.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...