Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema uongozi bora ni nguzo ya maendeleo endelevu ya nchi yetu, hivyo basi ni jukumu letu sote kama taifa kuhakikisha tunakuwa na viongozi bora wenye sifa na uwezo wa kuongoza kimkakati (Strategic Leadership).

Amesema hilo litafanikiwa kwa kuwa na mikakati thabiti ya kuwajenga na kuwaendeleza viongozi na kwamba mikakati hiyo ni pamoja na kuwa na programu maalumu za kuendeleza viongozi wa ngazi za juu na wanaochipukia katika sekta ya umma na bila kuacha nyuma sekta binafsi na Asasi zisizo za Kiserikali.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo leo Mei 16,2025 alipokuwa akizungumza katika mahafali ya Nane ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania ambapo mgeni rasmi alikuwa Mke wa Rais wa Finland Suzanne Innes-Stubb.

Akieleza zaidi Waziri Simbachawene amesema anafahamu Taasisi ya UONGOZI imeanza maandalizi ya kuwa na programu maalumu ya kuwezesha viongozi chipukizi (emerging leaders programme). Viongozi hao ni muhimu kwani wana kipindi kirefu cha kutumikia taifa letu wakati wa sasa na baadaye.

Hivyo amesema kuwaandaa na kuwajenga mapema kutaisaidia Serikali kuwa na kundi la Viongozi ambao wanaweza kupatikana pale watakapohitajika kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi."Naiopongeza Taasisi ya UONGOZI kwa kutambua umuhimu wa kuwa na programu hii kwa viongozi chipukizi."

Pia amesema dhima kuu ya maadhimisho ya mahafali hayo ya nane ya programu za uongozi ni Kukuza Uongozi wa Mabadiliko kwa Maendeleo Endelevu Barani Afrika.

"Dhima hii ni muhimu kwetu sote kwani uongozi wa mabadiliko unazidi kutambuliwa kama msingi wa kufikia Maendeleo Endelevu ya kijamii na kiuchumi, haswa katika muktadha wa Kiafrika.

"Agenda ya Umoja Wa Afrika ya Mwaka 2063 inaonesha Viongozi wana changamoto kubwa ya kujenga Bara la Afrika lenye taswira bora zaidi yenye maono ya Afrika tunayoitaka kwa kupunguza vikwazo vinavyorudisha nyuma maendelea ya Bara la Afrika.

"Hivyo, Tanzania na Afrika kwa ujumla inahitaji viongozi wa kimageuzi katika kuhamasisha juhudi za pamoja kuelekea kutimiza malengo ya pamoja kwa kuhamasisha uvumbuzi, kuongoza mabadiliko katika nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuandaa na kutekeleza Sera zinazokuza maendeleo jumuishi na endelevu ya Bara letu la Afrika."

Waziri Simbachawene amesema viongozi wa kimageuzi wana sifa ya kuwa na maono ya kuleta mabadiliko; wana uwezo wa kufanya maamuzi ya kimkakati, kuibua fursa mpya za Maendeleo, kuwasilisha na kushawishi mipango ya muda mfupi na mrefu ya kukuza uchumi na kuboresha hali ya maisha ya jamii zetu.

Hivyo ni matumaini yake mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuwa na maono, kusimamia utekelezaji wa mipango yetu pamoja na kupima na kufanya mapitio ya matokeo ya utekelezaji wake.

Aidha, ni matumaini yake pia watakuwa na uwezo mkubwa wa kutambua fursa na kuchangia katika kuweka mazingira mazuri ya kiuongozi yatakayochochea kuleta maendeleo endelevu nchini mwetu.

"Mafunzo mliyoyapata yawafanye kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo yenu ya kazi, na tunaamini mtakwenda kukuza na kuimarisha utawala bora kwa kufuata haki, sheria, kanuni, miongozo na taratibu tulizojiwekea, kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ubunifu na kuimarisha utendaji wa kazi ili kulisaidia taifa kufikia malengo tuliyojiwekea."

Pia amesema ili kufikia malengo makuu ya kuleta Maendeleo Endelevu Afrika, ametoa rai kwa Taasisi ya UONGOZI kuongeza kasi ya kupanua wigo wa Programu zake ili ziwafikie viongozi wengi zaidi wa Afrika.

Katika kuhakikisha programu hizo zinakuwa jumuishi na endelevu Barani Afrika mfumo bora na rafiki wa kuchangia gharama uandaliwe. "Ninatambua kuwa mmeshaanza kufanya hivyo na leo tuna wahitimu kutoka nchi nyingine za Afrika. Ninashauri tuongeze jitihada hizi ili kukuza uongozi wa mabadiliko na kuchangia Juhudi za mapinduzi ya kiuchumi barani Afrika."

Kuhusu suala la uratibu wa shughuli za Serikali, pamoja na uratibu wa miradi ya maendeleo umekuwa na changamoto nyingi zinazoathiri ufanisi. "Hili nililisema mwaka jana katika mahafali ya saba.

"Naomba leo nirudie tena kutoa rai kwenu, huko muendako mkasaidie kutafuta namna bora zaidi za kuratibu utekelezaji wa miradi katika njia itakayosaidia matumizi ya rasimali fedha na watu ili ilete matokeo makubwa na chanya. Kama mnavyofahamu, Serikali inawekeza pesa nyingi sana katika miradi hiyo ili kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi.

" Jambo hili litawezekana kama tutaimarisha mawasiliano na mahusiano na wadau wetu wa masuala ya maendeleo ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,"amesema na kufafanua ameelezwa wahitimu wamefundishwa umuhimu wa ubunifu na uvumbuzi, uthubutu, namna ya kuongoza watu na kusimamia rasilimali, kushirikiana, kuheshimiana na kutenda haki.

Pia wamefundishwa masuala muhimu ya maadili na utawala bora pamoja na athari za rushwa katika kutekeleza majukumu yenu kama watumishi." Yote haya yatoshe kusema sasa tunataka kuona utumishi bora wenye misingi imara na thabiti ya kiuongozi.

" Hatutegemei kuona mnaowaongoza au nyie wenyewe mkijihusisha na masuala ya rushwa, ubadhilifu, uzembe, uvivu na vitendo vya unyanyasaji ndani na nje ya kazi. Tunatarajia ninyi muwe chachu na mstari wa mbele wa mabadiliko kwa sababu mmepata fursa ya kupata mafunzo haya muhimu."




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...