Mkaguzi Mkuu wa Nje, Bw. Alfa Stanley, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 12, 2025 mara baada ya kufungua mafunzo ya wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) pamoja na asasi za kiraia (CSO).jpeg)
.jpeg)
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bw. Focus Mauki akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya mafunzo yaliyotolewa leo Mei 12, 2025.
OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) leo, Mei 12, 2025, imefungua mafunzo maalum kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika ya kiraia (CSOs), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mafunzo haya yanalenga kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma na kuongeza ushiriki wao katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.
Akifungua mafunzo hayo, Mkaguzi Mkuu wa Nje, Bw. Alfa Stanley, ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kusoma taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo huwasilishwa kwa Rais na Bunge, kisha kuwekwa wazi kupitia tovuti rasmi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi: www.nao.go.tz.
Bw. Stanley amesema mafunzo haya yatasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu kwa wananchi kwa kutumia lugha rahisi na michoro inayoeleweka kwa urahisi. Pia, amesema mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Ofisi ya CAG kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa matumizi hayo.
Ameongeza kuwa kupitia toleo maalum la Mwananchi kuhusu ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/2024, wananchi wataweza kupata uelewa wa kina kuhusu taarifa za ukaguzi na matumizi ya fedha za umma. Toleo hilo linapatikana kwenye tovuti ya NAOT na limeandaliwa kwa lugha nyepesi na michoro ya kueleweka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bw. Focus Mauki, amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa NGOs na CSOs kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha, Mbeya, na Dar es Salaam
Mada zinazofundishwa ni pamoja na:
Mchango wa Mpango Mkakati wa Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji wa NAOT katika kuimarisha uwajibikaji.
Malengo, majukumu na mbinu za Divisheni ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ukaguzi wa ufanisi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Uandaaji na uwasilishaji wa ripoti kutoka Kitengo cha Huduma za Kiufundi za Ukaguzi (TSSU).
Amesema lengo la mada hizo ni kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kuwajibika kwa kuuliza maswali, kuhoji matumizi ya fedha za umma na kushiriki katika mchakato wa ufuatiliaji.
Rehema Mwanteba kutoka shirika la Melisa amesema atatumia mafunzo haya kuwaelimisha wanawake kuhusu namna ya kuhoji mapato na matumizi ya fedha za maendeleo katika kata na vijiji vyao.
Naye Kalama Dickson kutoka Agenda Participation Initiative amependekeza kuwepo kwa mijadala ya mara kwa mara kati ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na wananchi kupitia taasisi za kiraia ili kujadili umuhimu wa uwazi na ushiriki wa jamii katika usimamizi wa fedha za serikali.
Amesisitiza kuwa uwajibikaji na uwajibishwaji unapaswa kuimarishwa hasa pale fedha za serikali zinapotumika bila tija katika miradi ya maendeleo au huduma zinazotolewa kwa jamii.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo wakiwa kwenye yaliyoandaliwa na ofisi ya Taifa ya ukaguzi.
Picha za Pamoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...