Madaba_Ruvuma.
Wanandoa wametakiwa kuwa waangalifu na kuchukua muda kutathmini mazuri waliyojengea katika ndoa zao kabla ya kusikiliza maneno ya watu wa nje wasiokuwa na nia njema. Ushauri huu umetolewa ili kuzuia maamuzi ya haraka ya kuvunja ndoa ambayo mara nyingi husababisha madhara makubwa kwa familia, hasa kwa watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Fedric Makamba, wakati wa utoaji wa elimu ya msaada wa kisheria na elimu ya uchaguzi katika vijiji vya Gumbiro, Ngadinda na Lituta, wilayani Madaba, Ruvuma, Mei 12, 2025.
Makamba amesema kuwa migogoro mingi ya ndoa inatokana na ushawishi wa watu wa pembeni ambao hutoa taarifa zisizo sahihi, na kuwasihi wanandoa kujadiliana kwa amani wanapokumbwa na matatizo. Ameeleza kuwa pale wazazi wanapotengana kwa uhasama, watoto huathirika zaidi kwa kukosa mwelekeo na malezi ya pamoja.
Kuhusu urithi, Makamba amesema watoto wote wana haki ya kurithi kutoka kwa mzazi wao awe ndani au nje ya ndoa lakini kila mtoto hurithi mali ya mzazi mmoja tu. Hii husaidia kuweka uwiano wa haki kulingana na mchango wa kila mzazi katika maisha ya familia.
Amehimiza pia ndoa zifungwe kisheria ili kuondoa mkanganyiko wa kimirathi au haki za ndoa, akibainisha kuwa ndoa ya kimila, ya kidini na ya kiserikali ndizo zinazotambulika kisheria. Aliongeza kuwa wenza wanaoishi pamoja kwa miaka miwili mfululizo wanaweza kutambuliwa kisheria kama wanandoa, hata kama hawana nyaraka rasmi.
Sababu za kisheria za kuvunjika kwa ndoa, kwa mujibu wa Makamba, ni pamoja na uzinzi wenye ushahidi, ukatili mkubwa, ugonjwa wa akili au kushindwa kushiriki tendo la ndoa. Hata hivyo, ndoa isiyodumu zaidi ya miaka miwili haitakiwi kuvunjwa isipokuwa kuwe na ushahidi wa ukatili mkali.
Iwapo wanandoa watashindwa kuelewana, wanapaswa kwanza kuelekezwa kwenye Baraza la Usuluhishi la Kata kabla ya kufikishwa mahakamani. Lengo la sheria, amesema Makamba, si kuvunja ndoa, bali kujenga familia zenye maelewano.
Aidha, watoto chini ya miaka saba hukaa na mama baada ya wazazi kutengana, isipokuwa pale mama akiwa na tabia mbaya inayotambulika wazi. Watoto wakishakuwa na umri mkubwa, hupewa nafasi ya kumchagua mzazi wa kuishi naye. Pia imeelezwa kuwa ni kosa kwa mzazi yeyote kumzuia mwenzake kumuona mtoto, kwani malezi ni jukumu la pamoja.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Hassan Linyama amesema kuwa baada ya kifo cha mume au mke, mume au mke aliyebaki pamoja na watoto wa ndoa ndio warithi wa kwanza. Ikiwa kuna watoto wa nje ya ndoa, mgawanyo hufanyika kwa kuzingatia kwamba wanarithi sehemu ya mzazi wao tu.
Linyama ameeleza kuwa usuluhishi unaweza kufanyika ndani au nje ya mahakama, na endapo maelewano yatafikiwa, shauri linaweza kuondolewa mahakamani. Kwa ndoa za kidini, mgawanyo wa mali hufuata taratibu za kidini, kwa idhini ya mahakama.
Naye Haruna Matata kutoka wizara hiyo, amefafanua kuwa mali zote zilizopatikana ndani ya ndoa ni za pamoja bila kujali nani alichangia zaidi, lakini mali za mtu kabla ya ndoa hubaki kuwa zake binafsi.
Wananchi wa Gumbiro wameipongeza serikali kwa elimu hiyo, wakisema imewaelimisha kuhusu haki na wajibu wao katika ndoa na familia. Wameomba mabaraza ya kimila yaanzishwe tena kusaidia jamii kulinda maadili na kutatua migogoro kwa haki.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea na inalenga kufikia kata zote nane za Halmashauri ya Madaba hadi Mei 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutoa elimu kuhusu haki za ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia, uchaguzi na utawala bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...