-Maboya 32 yawekwa katika mipaka ya Makulia ya Samaki

-Vifaranga vya Samaki 10,000 vya pandikizwa kwenye Mwalo wa Shadi Ziwa Victoria.

Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), imezindua Rasmi zoezi la kulinda Mazalia ya Samaki kwa kuweka maboya 32 kwenye mipaka ya maeneo maalumu yaliotengwa, kama alama ya kubainisha maeneo ya mazalia na makulia ya Samaki ambayo wavuvi wataweza kubaini maeneo hayo ambayo hayaruhusiwi kuvua, ikiwa ni moja ya njia ya kudhibiti Uvuvi haramu kwenye maeneo hayo maalumu yaliotengwa katika Ziwa hilo.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa, Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema swala la kuweka alama katika maeneo mahususi yaliobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki ni takwa la kikanuni, na maeneo haya yamebainishwa kwa kushirikiana na Maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi.

“Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji amenituma kuja kuweka alama za maboya kwenye maeneo yalioainishwa kama mazalia ya Samaki na vilevile kuja kupandikiza vifaranga vya samaki 10,000 katika mwalo wa Shadi, hapa Ziwa Victoria, japo tayari tulishapandikiza Vifaranga 1,231,000 katika Ziwa Ikimba mkoani Kagera” ameseama Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede amesema hategemei kuona wavuvi wakiharibu au kuvua Samaki katika maeneo haya yaliyobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki, na kuwataka Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kusimamia na kutoa taarifa pamoja na kuwaelimisha wavuvi kutofika sehemu hizo kwani swala la kulinda Rasilimali za uvuvi ni la kila mwananchi.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema Sekta ya Uvuvi inatoa fursa ya uvuvi kwa mwananchi, na kuna takribani mahitaji ya samaki tani laki saba kwa mwaka, ambayo inahitaji wadau wajitokeze katika kuwekeza na kuzalisha ili kuweza kufikia lengo ili tusiwe chini kwa ajili ya kuongeza pato la mtu moja na pato la Taifa kiujumla.

Dkt. Mhede amesema Serikali ina mpango kabambe wa miaka kumi ulioanzishwa mwaka 2022 na utaenda mpaka mwaka 2037 kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inachochea mapinduzi ya uchumi wa Buluu nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh amesema mkakati wa kulinda mazalia ya Samaki ni mkubwa kwa sababu katika maeneo ya ziwa na bahari kuna changamoto nyingi ikiwemo mambo ya athari za tabia ya nchi na ongezeko la watu linalopelekea mahitaji ya samaki kuongezeka na samaki kupungua, ndio maana Wizara imeamua kuchukua hatua katika kulinda rasilimali za uvuvi kwa kulinda mazalia ya samaki.

Pia, Prof. Sheikh, amesema huu ni mkakati endelevu, kwani kuna maeneo zaidi ya mia ambayo ni mazalia ya samaki ambayo yanahitaji kuwekewa maboya, na uwekaji huu umekuwa shirikishi kwa kuwashirikisha wadau wa uvuvi na wamekubali kulinda maeneo haya ya mazalia.

Halikadhalika, Prof. Sheikh amebainisha kuwa maboya haya yana ubora mkubwa na yana uwezo wa kuishi kwa miaka 80 kama yakitunzwa vizuri na yametengenezwa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, ili kusaidia katika uzalishaji wa samaki katika Ziwa Victoria.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Nassoro Mkilagi ameshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuleta maboya katika Ziwa Victoria ambayo yatasaidia katika Uzalishaji wa Samaki na kukuza shughuli za Uchumi Mwanza pamoja na Tanzania na kupungua shughuli za Uvuvi haramu nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, akizungumza na wavuvi wa Ziwa Victoria na wadau wa Sekta ya Uvuvi, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki,  Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Nassoro Mkilagi, akitoa neno la shukrani kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki,Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.
Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, akielezea lengo la kuweka maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (katikati), akiwa kwenye Boti tayari  kwa kwenda kuweka Maboya na kupandikiza Vifaranga vya Samaki katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani.
Wadau wa Sekta ya Uvuvi wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki,  Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...