- NI BAADA YA TRUMP KUFUTA MISAADA

Na Seif Mangwangi,Arusha

MTANDAO wa utetezi wa Haki za binaadam (THRDC), umesema sehemu kubwa ya watanzania watashiriki kwenye uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu bila ya kupewa elimu ya Uraia kufuatia Serikali ya Marekani kufuta misaada nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa amesema asasi nyingi nchini zimekuwa zikitegemea msaada kutoka serikali ya marekani kupitia miradi yake ya Demokrasia hivyo kufutwa kwa misaada hiyo kumeathiri miradi hiyo nchini.

Akizungumza katika kongamano la wiki ya Azaki 2025 linaloendelea Jijini Arusha alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utafiti iliyofanywa na THRDC juu ya athari za kukatwa kwa misaada na Serikali ya Marekani, Olengurumwa amesema asasi nyingi zimefunga ofisi zake na wafanyakazi kukosa ajira.

" Unajua mfadhili mkubwa duniani ni Serikali ya Marekani, asilimia 75 ya miradi yote duniani nchi hiyo ndio imekuwa ikiifadhili kwa hiyo kusitishwa kwa misaada hiyo kumeathiri pakubwa, sio tu asasi za kiraia hata wafanyabiashara wameathirika," amesema.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu wa madiwani, Wabunge na Rais wananchi watakosa haki ya kupewa elimu na hivyo utaathiri haki yao ya msingi ya kuelimishwa na kujua umuhimu wa kujitokeza kuchagua viongozi sahihi lakini hata kugombea hususani wanawake.

" Misaada ya marekani ndio imekuwa ikisaidia sekta za afya kwa wale wanaotumia dawa za ARV ambao wameathirika na sasa tunaona Serikali imeamua kutafuta pesa na kununua dawa hizo, kuna miradi ya kilimo, elimu n.k yote hiyo imekufa," amesema

Olengurumwa amesema ili kukabiliana na tatizo hilo la ukosefu wa fedha ni muda wa kushauri wadau wa Maendeleo kuzipatia fedha asasi za hapa nchini moja kwa moja bila kutegemea washiriki wa wadau hao ambao mara baada ya misaada kuondolewa na wao wamelazimika kufunga ofisi na kuondoka.

" Tumeona wadau wetu wa maendeleo mfano USAID walikuwa wakitoa pesa kwa mashirika ya kimataifa yenye wakala wao hapa nchini na sisi kuzipata pesa kutoka kwa wakala hao ambapo baada ya Trump kuzuia misaada ya Marekani ikabidi wafunge ofisi, lakini kama ingekuwa ni fedha wanatupatia moja kwa moja kwenye asasj zetu leo hii tungeendelea kuwepo na kuona nini tufanye ili tuweze kuendelea kusaidia jamii yetu," amesema.

Amesema pia ni wakati wa viongozi wa azaki kuwashawishi wafadhili kuwapatia asilimia fulani katika fedha wanazotoa kwaajili ya kufanya uwekezaji ili siku misaada hiyo ikikata asasi zitaendelea kufanyakazi kupitia miradi itakayoanzishwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa asasi ya Hakielimu Tanzania Dkt John Kallaghe amesema ni vyema asasi ikatengeneza sera itakayoonyesha kati ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi, asilimia fulani hubakishwa kwaajili ya kufanyia uwekezaji na kwamba hiyo itasaidia kumweka wazi mfadhili.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...