Kampuni ya usafiri wa mtandaoni, Bolt, inaendelea kuongoza kwa kushikilia asilimia 70 ya soko la huduma za usafiri nchini. Mafanikio haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wake wa kuoanisha usalama, bei nafuu, na teknolojia bunifu inayokidhi mahitaji ya usafiri kwa tabaka mbalimbali za watumiaji.

Katika mahojiano ya moja kwa moja yaliyofanyika wiki iliyopita kupitia kituo kimoja cha redio hapa jijini Dar es Salaam, Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt kwa Tanzania na Kenya, alieleza kanuni 10 ambazo madereva waliofanikiwa huzifuata – licha ya kutokuwa sehemu ya sera rasmi za kampuni.

“Madereva wetu ni nguzo muhimu katika uchumi wa miji nchini Tanzania. Kwa mfano, tuna pikipiki nyingi kuliko magari, na nyingi hutumika kwa shughuli za kiuchumi. Hata wakati wa msimu wa mvua uliopita, mahitaji ya usafiri kupitia boda boda na teksi yaliongezeka hasa kwa abiria wanaokwenda kazini au wafanyabiashara wanaotoa huduma za usafirishaji wa bidhaa,” alisema Dimmy.

Kwa mujibu wa Bolt, mafanikio ya mfumo wao yanatokana na uwezo wa jukwaa lao kuunganisha madereva na abiria, kupangilia bei kwa usawa ili madereva wasinyonywe, na kuvutia abiria wengi wanaotafuta suluhisho la usafiri wa uhakika na salama. Hali hii imewafanya madereva wengi kuliona jukwaa hili kama chanzo madhubuti cha kipato.

Katika mahojiano hayo, Dimmy alibainisha kanuni 5 kuu ambazo madereva wanaofanikiwa huwa hawazipuuzi:

1. Usiwashe App Kama Hauko Tayari Kuchukua Abiria

Usipokuwa tayari kufanya safari, usijaribu kuwa hewani – hatua hiyo huathiri alama zako kama dereva. Wakati wa kula au mapumziko, zima huduma ya upatikanaji ili kuepuka kughairi safari au kukataliwa, hali inayoshusha kiwango chako cha utendaji.

2. Simu Yako Iwe Imesasishwa Kila Wakati

Hakikisheni app ya Bolt inafanya kazi vizuri kwa kuwa na simu iliyosasishwa – teknolojia ya kisasa inahitaji vifaa vya kisasa.

3. Tambua Maeneo ya Joto na Vipindi Vyake

Fanya kazi kwa akili, si kwa nguvu tu. Asubuhi elekea maeneo ya makazi kwenda katikati ya jiji (kama vile Mikocheni hadi Posta), mchana zunguka maeneo ya ofisi za serikali na migahawa, jioni kuwepo karibu na baa, mall na vituo vya mabasi.

4. Huduma ya Nyota Tano = Bakshishi Nzuri + Wateja Kurudi Tena

Tofauti huletwa na huduma ndogo ndogo: gari safi, hewa nzuri, usigombane au kulalamika kuhusu njia ya safari, na kuwa na mtazamo chanya wa kibiashara – changamoto ni sehemu ya kazi.

5. Usikae Sana Bila Safari

Kama upo eneo moja kwa zaidi ya dakika 15 bila kupata safari, hama haraka na elekea eneo lenye abiria. Kusalia maeneo ya “kufa” kunapunguza kipato chako kwa saa.

Kanuni zingine zinazoshauriwa na kampuni ni;

6. Fuatilia Taarifa za Bolt kwenye Makundi ya WhatsApp ya Madereva

Hapa ndipo taarifa mpya zinazopatikana: maeneo yenye abiria wengi, masasisho ya app, na taarifa kuhusu matukio makubwa. Habari ni nguvu.

7. Epuka Kughairi Safari – Isipokuwa Ikiwa ni Muhimu Sana

Kughairi mara kwa mara kunaharibu kiwango chako cha kupokea safari, hupunguza nafasi za kupata safari mpya, na kuathiri uonekano wako kwenye app.

8. Epuka Safari Fupi Kwenye Eneo la Msongamano

Safari chini ya TZS 3,000 maeneo kama Kariakoo au Posta ni hasara. Kubali tu kama uko kwenye “Boost” au kuna uwezekano wa safari kubwa baadaye.

9. Kuwa Mstaarabu Lakini Thabiti Kuhusu Usalama

Ukikumbana na abiria anayevunja kanuni (kama kupakia abiria wengi kuliko kawaida au njia hatarishi), shikilia sera kwa utulivu. Wateja wanaheshimu madereva wanaojali usalama.

10. Lenga Safari Zinazofuatana Bila Kupumzika

Baada ya kumaliza safari, usizime app mara moja. Kubaki hewani maeneo ya mall, vyuo, au maeneo ya biashara huongeza nafasi ya kupata safari nyingine mara moja.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...