Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIBU Tawala Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam Warda Abdallah ameipongeza Shule ya Kimataifa ya Monti kwa kuibua na kulea vipaji vya watoto ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia katika dunia ya sasa.

Pia ameeleza kufarijika na malezi pamoja na elimu ya kisasa wanayopatiwa watoto hao na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa shule hiyo inayotumia mtaala wa kimataifa wa Cambridge unaozingatia kiwango cha kimataifa cha elimu na kutambuliwa na vyuo vikuu na waajiri kote duniani.

Katibu tawala huyo amebainisha hayo mwishoni mwa wiki katika sherehe za mahafali ya nne ya shule hiyo ya awali na msingi iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa wanafunzi waliohitimu elimu ya awali na kutarajiwa kuanza darasa la kwanza.

“Tumewasisitiza kuwakumbusha umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto na hasa ukiangalia dunia inapoenda tunahitaji sana mawasiliano ya karibu kati ya mzazi na mwalimu ili kumlinda na kujua kipaji chake ni nini,” amesema.

Aidha, akizungumzia matumizi ya akili mnemba (AI) ambayo watoto hao hufundishwa namna ya kuitumia kwa usalama na usahihi huku walimu wao nao wakifundishwa namna ya kuitumia kuandaa mpango kazi wa masomo, DAS Warda amesema IA ina faida kubwa.

“Inawasaidia watu kuwa wabunifu kwa kupata ule uwezo wa haraka kufikiri lakini changamoto kubwa tunahofia tusije kuzalisha taifa ambalo si wabunifu, sio watu wa kufikiri kwa kutumia akili zao, nimewasihi wazazi kufuatilia kwa karibu matumizi ya zana hizi za kiteknolojia,” amesema.

Akizungumzia mahali hayo, Mkurugenzi Mkuu na mmiliki wa shule hiyo, Fatma Fernandes amesema shule hiyo inampokea mtoto mwenye umri kuanzia mwaka mmoja na kuendelea kisha kumlea na kumkuza kielimu hadi anapofikisha umri wa miaka mitano ndipo anapoanza darasa la kwanza.

“Kwa elimu ya msingi watoto wanasoma kwa miaka sita. Shule ina matarajio makubwa ikiwemo kujenga miundombinu inayolenga kuunga mkono vipaji vya watoto. Mfano tunajenga ‘swimming pool’ kwa wale wanaopenda kujifunza kuoegelea, pia tutajenga viwanja vya mchezo wa mpira wa kikapu na tenesi, pia tunajenga kampasi Madale ambayo itakuwa ya msingi na sekondari na ni kutwa na bweni,” amesema na kuongeza;

“Tulianzisha shule kwa lengo la kuwahudumia watoto wa aina yoyote mfano wenye usonji kwa sababu shule inalenga kumuelewa mtoto ndipo tunajikita kumhakikisha kila kitu anapata kwa maendeleo yake ya ukuaji”.

Aidha, amesema wamejikita kuhakikisha watoto wanasoma kompyuta kupitia maabara ya kompyuta iliyopo shule hapo.

“Kuhusu matumizi ya AI hatujaangalia tu kwa mtoto lakini pia tumeangalia pia kwa mwalimu ili kurahisisha kazi ya ufundishaji. Kwa sasa kuna School AI ambayo tumeweka kwenye mifumo yetu ambayo inamsaidia mwalimu kumrahisishia kutengeneza mpango kazi wa masomo, mwalimu hatumii tena saa 40 kama zamani, kwa muda mfupi anaweza kutengeneza kila kitu anakwenda darasani na kuwafundisha watoto na kumuelewa,” amesema na kuongeza;

“Walimu wamejikita kuelewa AI na kuhakikisha watoto wetu wanaitumia kwa usalama. Kompyuta zetu zote zina mifumo ambayo ni salama kwa watoto kutumia”.

Kwa upande wake mmoja wa wazazi wenye watoto shuleni hapo, Kaley Milao alieleza kuridhishwa na uwezo wa watoto walionesha katika masomo pamoja na kufikiri.

“Tunategemea makubwa kwani wanafungua kampasi kule Madale. Utakuwa ni muendelezo mzuri kwa sababu AI au teknolojia haiepukiki, lazime tuende nayo tuone namna gani tunaitumia kutufaidisha sisi.

“Sasa kwa mtoto au kizazi hiki cha watoto ambacho AI imeanza na inakua ni kuwawezesha kuishi katika mazingira hayo ili kuwasaidia na sio kuwaharibu cha msingi tuwasimamie kwa karibu na sio kumtenga mtoto na dunia inavyoenda.

Katibu tawala wilaya ya Kinondoni - DAS, Warda Abdallah akimpatia cheti mmoja wa watoto waliohitimu elimu ya awali katika Shule ya Kimataifa ya Monti iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam. Mahafali hayo ya nne shule hiyo inayotumia mtaala wa Kimataifa wa Cambridge, yamefanyika mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi Mkuu na mmiliki wa shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes akifuatilia maonesho ya vipaji vya watoto waliohitimu elimu ya awali katika shule hiyo. Mahafali hayo ya nne shule hiyo inayotumia mtaala wa Kimataifa wa Cambridge, yamefanyika mwishoni mwa wiki Mikocheni jijini Dar es Salaam.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...