Na Mwandishi Wetu

Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni Tanzania (CEOrt Roundtable) lililowakutanisha viongozi wakuu kutoka sekta ya fedha, sekta binafsi, na taasisi za maendeleo limefanyika jijini Dar es Salaam likiwa na kaulimbiu ya “Kuhamasisha Rasilimali kwa Mabadiliko ya Kijani,”.

Kongamano hilo liliangazia mbinu bunifu na changamoto muhimu katika upanuzi wa fedha ( green finance) ili kuharakisha ajenda ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Kongamano hili lilidhaminiwa kwa pamoja na IUCN, Benki ya NMB, Benki ya KCB Tanzania, na WWF Tanzania, jambo linaloashiria mshikamano unaokua kati ya sekta za fedha katika kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu wa kifedha.

Bi Santina Benson, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, alifungua kongamano hilo kwa kusisitiza umuhimu wa uwezeshwaji wa kifedha kama nguzo ya maendeleo ya taifa.

“Uwezeshwaji wa kifedha —ni msingi wa biashara endelevu na maendeleo ya kitaifa,” alisema. “Tunapaswa kuacha nadharia na kuhakikisha mitaji inawafikia wafanyabiashara walioko tayari kuwekeza katika ukuaji unaozingatia mazingira.”

Benson alitambua mafanikio yaliyopatikana kupitia pamoja na mambo mengine hati fungani (bonds) na utoaji wa mikopo yenye masharti rahisi kwa wadau wa maendeleo wakiwemo wakulima.

Alisisitiza haja ya kuwepo kwa mazingira bora zaidi ya kuwezesha mabadiliko hayo.

Viongozi kutoka taasisi kuu za kifedha walisisitiza kauli hizo:

Peter Nalitolela, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), alieleza maendeleo kupitia hati fungani, akisisitiza haja ya kuongeza ushiriki na kuimarisha mifumo ya taasisi ya kifedha ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Naye Innocent Yonazi, Mkuu wa Mahusiano na Wawekezaji wa Benki ya NMB, alisisitiza umuhimu wa fedha jumuishi, akitaja nafasi muhimu ya wanawake, vijana, na jamii zilizo pembezoni katika kujenga uchumi thabiti wa kijani.

“Kuchelewesha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutazidisha umaskini na ukosefu wa chakula,” alionya.

Gabriel Lekundayo, Mkurugenzi wa Benki ya Biashara wa KCB Bank Tanzania, alionyesha jinsi taasisi za kifedha zinavyojielekeza kwenye miradi yenye mnepo wa tabianchi, hasa katika sekta za kilimo na miundombinu.

Maoni kutoka katika kongamano hili yanaendana na vipaumbele vya hivi karibuni vya serikali.

CEOrt inaendelea kujitolea kuhamasisha uongozi wa sekta binafsi katika kushiriki ukuaji wa uchumi kupitia —mpango unaolenga kutafsiri sera za taifa za tabianchi kuwa uwekezaji wenye tija kutoka sekta binafsi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...