Aliyekuwa Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Matogoro, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Issa Mkwawa, amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Songea Mjini kupitia tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao. Hatua hiyo imekuja baada ya kutafakari kwa kina juu ya mahitaji ya wananchi wa jimbo hilo na nafasi ya chama katika kuwaletea maendeleo ya kweli.
Mkwawa amesema amejipima na kuona kuwa anatosha kuwaongoza wananchi wa Songea Mjini kwa mafanikio, akieleza kuwa anayo dhamira ya dhati ya kushirikiana na viongozi waliopo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan katika maeneo ya kilimo, masoko, ajira kwa vijana, ujenzi wa viwanda na kuimarisha mshikamano ndani ya CCM.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Mkwawa amesisitiza kuwa Songea inahitaji mabadiliko ya kweli na ya kimaendeleo ambayo yataendana na kasi ya dunia ya sasa. Ameeleza kuwa anaamini ana maono na uwezo wa kuhakikisha Songea Mjini inakuwa kitovu cha uchumi wa mkoa wa Ruvuma kupitia utekelezaji wa sera zenye tija na usimamizi madhubuti wa rasilimali.
Ameongeza kuwa uzoefu alioupata akiwa diwani utamsaidia kuwa kiongozi wa karibu na wananchi, mwenye kuelewa mahitaji yao halisi. Mkwawa ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono katika safari yake ya kugombea ubunge, huku akiahidi kuwa sauti ya wanyonge, mtekelezaji wa ilani ya chama, na kiungo imara kati ya serikali na wananchi wa Songea Mjini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...