Dar es Salaam, Tanzania – 19 Juni 2025

Stanbic Bank Tanzania na Vodacom Tanzania leo wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) ya kihistoria ya miaka mitatu ili kusaidia Twende Butiama Cycling Tour — kampeni ya kitaifa inayochanganya michezo, uendelevu wa mazingira, na maendeleo ya kijamii. Kupitia ushirikiano huu, Stanbic Bank imejitolea kuchangia TZS milioni 300 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ili kupanua wigo wa msafara huu kote nchini Tanzania.

Msafara huu hufanyika kila mwaka kwa heshima ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na zimekuwa alama ya mshikamano na hatua ya pamoja kwa ajili ya mabadiliko. Msafara wa Twende Butiama huwakutanisha waendesha baiskeli, viongozi, na jamii mbalimbali nchini katika dhamira ya pamoja ya kukuza elimu, huduma za afya, na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, alisisitiza tena dhamira ya benki hiyo katika kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Tanzania. “Tunapoadhimisha miaka 30 ya huduma ya Benki ya Stanbic hapa Tanzania na Vodacom wakiadhimisha miaka 25 ya kuunganisha jamii, ushirikiano huu ni zaidi ya ishara ni uthibitisho wenye nguvu wa dhamira yetu ya pamoja kwa maendeleo ya taifa. Kwetu Stanbic, tunaamini kwamba Tanzania ni nyumbani kwetu, na tupo hapa kuendesha maendeleo yake. Juhudi za mwaka huu kupitia mpango wa Twende Butiama unaolenga kufikia shule 10, kupanda miti 50,000, na kuboresha maisha ya Watanzania zaidi ya 700,000 ikiwa ni watoto, vijana, wazee hii inaonyesha kiwango na athari ya dhamira hiyo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, aliipongeza ushirikiano huo kama ushuhuda wa muda muafaka wa ushirikiano wenye malengo ya kijamii. “Mchango wa Stanbic Bank unatuwezesha kuinua Twende Butiama hadi ngazi ya juu zaidi. Kwa miaka kadhaa, msafara huu umekua na matokeo athari kubwa katika shule za vijijini, huduma za afya, na kampeni za kuhifadhi mazingira. Ushirikiano huu unaimarisha maono yetu ya pamoja ya kuwawezesha Watanzania kupitia maendeleo jumuishi na endelevu.”

Ahadi ya TZS milioni 300 itasaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika njia ya msafara huu, ikiwemo kuboresha mazingira ya kujifunzia, kutoa huduma za afya kwa jamii vijijini, na kurejesha ikolojia ya Mlima Kilimanjaro kupitia kampeni za upandaji miti. Twende Butiama pia ni jukwaa la kushirikiana kati ya sekta binafsi na umma, kuhamasisha vijana, na kuunganisha vizazi, ambapo waendesha baiskeli wenye umri kati ya miaka 14 hadi 75 hushiriki kila mwaka.

Gabriel Landa, Mwanzilishi wa Msafara wa Twende Butiama aliongezea“Yote tunayoyafanya kama Twende Butiama ni kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kutekeleza maono yake hasa katika elimu, mazingira, na afya kwa jamii. Tunawashukuru kwa dhati wadau waliotuunga mkono tangu mwanzo, pamoja na wale wanaoendelea kushirikiana nasi kama Stanbic na Vodacom. Ushirikiano huu umetuwezesha kupanua wigo wa kampeni hii na kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi. Tunawakaribisha wadau wengine kujiunga nasi, sambamba na waendesha baiskeli kutoka ndani na nje ya nchi. Mwaka huu tunafurahi kuwa na washiriki kutoka Zambia, Congo, Burundi, Malawi na mataifa mengine. Tunaamini kwa kushirikiana, tutaweza kufanikisha azma yetu ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa jamii.”

Kadri maandalizi ya toleo la mwaka 2025 yanavyoendelea, ushirikiano huu kati ya Stanbic Bank na Vodacom Tanzania unaashiria hatua muhimu ya kuenzi urithi wa Nyerere kupitia vitendo, mshikamano, na dhamira ya kitaifa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...