Masasi-Mtwara.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini, umekabidhi mbao 5,000 zenye thamani ya shilingi milioni 37 kwa Wilaya ya Masasi, kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya miundombinu ya elimu, Mbao hizo zitatumika katika ujenzi wa madarasa, mabweni pamoja na utengenezaji wa madawati kwa shule mbalimbali wilayani humo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Juni 28, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TFS Prof. Dos Santos Silayo, Kamanda wa Jeshi la Uhifadhi TFS Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya TFS katika kuendeleza usimamizi endelevu wa rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema msaada huo ni dhamira ya TFS ya kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa hasa misitu na nyuki, zinasimamiwa kwa njia endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni hatua ya kuonyesha shukrani kwa wananchi kwa kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na TFS katika jukumu kubwa la kulinda, kuhifadhi na kuendeleza mazingira ya wilaya hiyo.
Ameeleza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha kuwa anatunza rasilimali za misitu huku akihimiza walimu, wanafunzi, viongozi wa dini na jamii, kuendeleza utamaduni wa kupanda miti ya kivuli na matunda katika maeneo ya shule, zahanati, na taasisi nyingine, ili kusaidia kuimarisha mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kasanda, amepongeza TFS kwa mchango huo muhimu na kuahidi kuwa mbao hizo zitatumika kama ilivyokusudiwa. Alitumia nafasi hiyo pia kuwataka TFS kuendeleza mapambano dhidi ya ukataji holela wa miti na uchomaji wa misitu kwa ajili ya mkaa, akisisitiza kuwa uharibifu huo wa mazingira hautaondoa umasikini bali utaongeza changamoto za kijamii na kimazingira.
Afisa Ugani na Uenezi kutoka TFS Kanda ya Kusini Anderson C. Besisila, amewataka wananchi wa Masasi kutumia nishati mbadala kama gesi na majiko banifu badala ya kuni na mkaa ili kusaidia kuhifadhi misitu, Pia amesisitiza umuhimu wa kutoanzisha moto usiodhibitika, akieleza kuwa moto ni adui mkubwa wa misitu.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Matankini Alkwini Julius Chitanda, ameishukuru TFS kwa msaada huo na kuahidi kuwa viongozi wa mtaa wake wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za uharibifu wa misitu, amebainisha kuwa msaada wa mbao hizo utaondoa changamoto ya upungufu wa madawati mashuleni, hivyo kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa Masasi.
Msaada huo kutoka TFS ni kielelezo cha ushirikiano wa dhati kati ya serikali na jamii katika kulinda rasilimali za Taifa, huku ukitoa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto ya miundombinu ya elimu. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa misitu kwa maendeleo endelevu ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...