Na Mwandishi Wetu

UTAFITI uliofanywa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuhusu wahitimu wake umeonyesha kuwa asilimia 59 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati wa kongamano la kuimarisha fursa za ajira na maendeleo endelevu ya Tanzania kaulimbiu ikiwa ni ‘ubunifu na ujasiriamali kwa ajira endelevu’

Mgeni mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye alimwakilisha Waziri Dk Selemani Jafo.

Alisema utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 20 ya wahitimu wake wamejiajiri wenyewe na asilimia 21 bado wanatafuta ajira.

“La kufurahisha asilimia 96 walionyesha utayari wao wa kuipendekeza CBE kwa wengine na matokeo haya yanatuonyesha kwamba CBE bado tunatoa elimu sahihi na tunaenda kuiboresha zaidi kuendana na wakati,” alisema

“Ufuatiliaji huo umesaidia kutujengea taswira nzuri kwenye jamii kama taasisi bora ya kuandaa wahitimu wenye uwezo chuo hiki pia kinaunganisha wahitimu na waajiri na mfano mwaka jana walipohitimu 100 waliomaliza usimamizi wa biashara waliajiriwa Shirika la Reli (TRC), alisema

Alisema hiyo inaonyesha kuwa elimu inayotolewa chuoni hapo inachochea ubunifu na inahitajika kwenye soko la ajira na wahitimu wengi wanauwezo wa kujiajiri wenyewe.

Prof alisema CBE imeanzisha utaratibu wa kuajiri baadhi ya wahitimu wanaofanya vizuri zaidi kwenye masomo yao kama walimu wa kujitolea chuoni hapo ambao wamekuwa wakifundisha na kusimamia wenzao.

“Wenye GPA zaidi ya nne huwa tunawahamasisha waombe nafasi hapahapa CBE na wakipata nafasi wanachukuliwa kwenye kampasi zetu zote na pamoja na kuboresha mitala yetu tuna uhusiano mzuri na taasisi binafsi na serikali na za nje ya nchi” alisema

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wahitimu wa zamani wa chuo hicho, Maeda Waziri alimpongeza Profesa Lwoga kwa mageuzi makubwa aliyofanya chuoni hapo.

“Mimi nilisoma hapa miaka mingi iliyopita, CBE haikuwa hivi ilivyo leo mambo mengi yamefanyika ya kitaaluma na hata majengo yameongezeka kwa kasi kubwa sana lazima tumpongeze Profesa Lwoga kwa kazi nzuri,” alisema

“Najivunia kusoma CBE kwani nimepata tuzo nyingi sana na kwa sasa Tanzania nzima mwanamke ambaye ni mkandarasi wa barabara daraja la kwanza niko peke yangu. Kwa hiyo mnaweza kuona sikwamba nilipata elimu tu hapa ila niliondoka na msingi mzuri sana,” alisema

Alisema bila kuwa na ujuzi wa biashara ambayo mtu anaenda kuifanya inakuwa ngumu sana kwake kufanikiwa hivyo elimu aliyoipata CBE ilimjengea uwezo wa kutambua fursa, kuzifanyia kazi na kukabiliana na changamoto.

“Elimu ya hapa ilinipa utambuzi wa kufanya mambo sahihi na siyo kwa hisia na ndiyo maana niliweza kufanya mambo makubwa na nimepata tuzo nyingi sana hapa nchini,” alisema 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...