Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Dk. Aneth Komba kwa kazi kubwa na nzuri wanazozifanya katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule zote nchini.

Majaliwa ameyasema hayo leo Juni 17,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa TET, maadhimisho yaliyokuwa na kauli mbiu ya 'Kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja'.

Maadhmisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa Soma kwanza TV, uzinduzi wa Mfumo wa Ufundishaji na Ujifunzaji wa Walimu (LMS) pamoja na uzinduzi wa Jalada la kitabu cha hadithi cha 'Bi Mkubwa na Wajukuze'.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema TET chini ya Dk. Komba na menejimenti yake hakika wamefanya kazi nzuri na wanapaswa kupongezwa kwa mafanikio makubwa waliyoyapata ikitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

"Leo tunapoadhimisha miaka 50 tupo hapa tukitembea kifua mbele kwa kazi nzuri ambayo imefanywa na TET, hii ni ishara kuwa mlichokifanya kwa miaka 50 ni kizuri na mnauhakika kuwa mtaendelea kufanya vizuri zaidi," amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Amesema katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia, TET imezindua Soma Kwanza TV, Mfumo wa LMS na Jalada la Kitabu cha 'Bi Mkubwa na Wajukuzu' ambalo linalengo la kujenga tabia ya watoto kupenda kusoma vitabu na kujifunza mbinu mpya kulinga na maendeleo ya teknolojia.

"Uaandaaji wa mifumo hii ni jambo moja lakini suala la muhimu ni kuhakikisha inatumika ipasavyo na kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwemo ya kuondoa changamoto zilizopo na kupunguza gharama za matumizi ya mitandao, nashukuru mmeanza na Airtel katika suala hili la mtandao na mpo katika mazungumzo na Vodacom," amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema TET inajitahidi kutoa elimu si kwa kutumia zile njia zilizozoeleka bali kwa kutumia njia za kidijitali ili kuendana na ukuaji wa teknolojia.

Aidha amesema chini ya uongozi wa Wizara ya Elimu kupitia TET inahamasisha uandishi bunifu wa riwaya, tamthiliya na hadithi za watoto kwa lengo la kuchochea watu binafsi kuandika vitabu.

"Tumefanya hivyo kwa kuanzisha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, lengo ni kuchochea watu wanaotaka kuandika washiriki si tu washinde bali vitabu vyao vichapishwe na viwe sehemu ya kukuza lugha ya kiswahili nchini," amesema

Kwa upande wake, Dk. Komba amesema serikali kupitia taasisi ya TET imeshirikiana na Shirika la Soma Kwanza Initiatives kuanzisha TET Soma Kwanza TV ambayo imelenga kuandaa na kurusha maudhui ya kielimu kwa saa 24 vikiwemo vipindi mbalimbali katika mtaala kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.

Amesema TV hiyo kwa sasa inapatikana katika king'amuzi cha Startimes Channel namba 105 na kwamba lengo kwa siku za baadae ipatikane kwenye ving'amuzi vyote ili kuweza kufikia walengwa wengi zaidi na kwamba wataanzisha TET Soma Kwanza Redio.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...