NA MWANDISHI WETU, PEMBA
BENKI ya NMB imewahakikishia wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa walioshiriki Kongamano la Uwekezaji Zanzibar lililoratibiwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kuwa iko imara kifedha kuwawezesha kushiriki Mapinduzi ya Kiuchumi visiwani humo na Tanzania kwa ujumla.
Uthibitisho wa uimara wa NMB ni kuingia kwa benki hiyo katika Klabu ya Kampuni Zenye Thamani ya Zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 1 Duniani, Faida Baada ya Kodi (Sh. Bil. 643), Gawio kubwa kwa Serikali (Sh. Bilioni 214) na tuzo kadhaa za kimataifa zikiwemo za Euromoney na Global Business and Finance.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya NMB, Bi. Linda Teggisa, wakati akitoa wasilisho kwa washiriki wa Kongamano hilo, lililowakutanisha wawekezaji zaidi ya 1,000 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na Afrika kwa ujumla, lililofungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Katika wasilisho lake kwa washiriki hao, Bi. Linda alisema, benki yake inajisikia fahari kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kukuza Uchumi wa Buluu, fursa iliyowapa nafasi ya kuzungumza na wawekezaji na kuwaonesha masuluhisho na huduma nzuri, muhimu na bora walizonazo kwa ajili ya wawekezaji.
“Sisi NMB tunalitumia wasilisho hili kuwaonesha washiriki uwezo wetu kama benki kwa upande wa masuluhisho tuliyonayo kwa wateja binafsi, wakubwa na taasisi za Serikali, ikiwemo uhamishaji wa fedha kwa ajili ya kuwezesha biashara kwa mtu aliyeko nje ya nchi ama aliye ndani anayenunua bidhaa nje ya nchi.
“Benki yetu ina mtaji wa takribani Dola za Marekani Bilioni 1.1, thamani inayoifanya kuwa benki ya kwanza nchini na ya pili kwa ukubwa Afrika Mashariki, tukiingia katika taasisi zenye thamani ya zaidi ya dola Bilioni 1 na siri ya mafanikio haya ni pamoja na uwekezaji katika teknolojia, ambako asilimia 96 ya miamala yetu hufanyika kidijitali.
“Sisi ni vinara wa suluhisho za kifedha nchini na tuna uimara na nguvu ya kutosha kusaidia uwekezaji na kuchochea Mpango Mkakati wa Seriakli ya Zanzibar katika kuboresha Maeneo ya Uwekezaji Micheweni na Zanzibar kwa ujumla, kama ilivypobainishwa na Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji,” alisema Bi. Linda.
Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Cocco Lagoon, Grzegorz Adamczak, akitoa wasilisho lake kwa washiriki, alisema NMB ni benki ambayo imejipambanua kiasi cha kuvutia hata wawekezaji walio nje ya mipaka ya nchi wanaofikiria kuja kufanya uwekezaji, na kwamba mafanikio yao na tuzo za kimataifa, zimewajengea thamani kubwa.
“Kulingana na rekodi na takwimu zake, imekuwa ni benki inayotoa mchango mkubwa katika ukuaji kiuchumi miongoni mwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa ngazi zote, kama ilivyo pia kwa wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa,” alichangia Adamczak ambaye aliitaja NMB kama benki sahihi kwa wawekezaji.
Kwa nyakati tofauti, katika mawasilisho yao, Safari Fungo ambaye ni Mratibu wa Markup, International Trade Center na Emilian Busara ambaye ni Mshauri wa Masuala ya Fedha, walisifu bunifu mbalimbali za NMB na kwamba udhamini na ushiriki wao katika Kongamano la Uwekezaji Zanzibar, ni fursa kwa washiriki kufanikisha malengo yao.
“Niko hapa kama Mchambua Mada wa Kongamano la uwekezaji, lakini naijua na kuifahamu vema NMB kutokana na ushiriki wangu katika ushauri wa masuala ya fedha nchini Tanzania, ndio benki kubwa inayoongoza kwa faida, mwaka jana tu ikipata faida baada ya kodi ya zaidi ya Sh. Bil. 600, lakini pia hivi karibuni ikitoa gawio kubwa zaidi.
“Pia, imetunukiwa Tuzo ya Benki Bora, Mlipa Kodi Mkubwa Zaidi na Mlipa Kodi Anayelipa kwa Wakati, ndio maana kama mshauri, sisiti kuwashauri wawekezaji walioshiriki kongamano hili na wengineo, kufanya kazi na NMB ikiwa itahitaji kuharakisha mafanikio ya uwekezaji wao katika miradi mbalimbali,” alibainisha Emilian.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...